
MWANAMKE aliyejulikana kwa jina la Maida Julius Mwashilindi, mkazi wa Tabata-Kimanga jijini Dar, amefariki dunia baada ya kudaiwa kuchomwa visu na mumewe, Steven Mwashilindi ambaye kwa sasa naye ni marehemu.
Katika tukio hilo lililojiri wiki iliyopita, Mwashilindi alidaiwa kujiua kwa kujinyonga baada ya kumchoma visu tumboni mkewe huyo ambaye alikuwa na hali mbaya.
Akizungumza na Ijumaa Wikienda, wikiendi iliyopita wakati wa kuuaga mwili wa Maida kwenye Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya kusafirishwa kwenda mkoani Songwe kwa maziko, mmoja wa ndugu wa familia hiyo ambaye hakutaka jina liandikwe gazetini alisema kuwa, Maida alifariki dunia alfajiri ya Oktoba 17, mwaka huu katika Wodi ya Kibasila hospitalini hapo. “Dada yangu alichomwa visu tumboni mpaka utumbo ukatoka nje na kisu kingine alichomwa maeneo ya kifuani Siku ya Jumamosi ya Oktoba 13.
“Yote hayo alifanyiwa na aliyekuwa mume wake kwa madai ya kuhisi kuwa mwenye nyumba waliyokuwa wanaishi na mkewe wamefanya njama ili wamtoe kwenye nyumba hiyo kwa kuwa walikuwa wanadaiwa kodi na yeye kuchukua uamuzi wa kumchoma visu mkewe. “Baada ya kuona mke wake amezidiwa na baada ya kuona hajafa, akajifungia chumbani kisha kujinyonga kwa kutumia kamba hadi akafariki dunia.
“Sasa tukiwa bado tupo msibani mkoani Songwe, tulipigiwa simu kuwa na dada yangu naye amefariki dunia, lakini kipindi hatujaondoka alikuwa anaendelea vizuri. “Ile siku ya tukio tulimpeleka Hospitali ya Tabata, pale tuliambiwa tumpeleke Amana, napo tukaambiwa tumlete hapa Muhimbili kwa kuwa hali yake haikuwa nzuri na utumbo ulikuwa nje.
“Baada ya kumfikisha hapa alipelekwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi kisha akawa anaendelea vizuri ndipo akahamishiwa wodi ya kawaida ya Kibasila. “Wakati akiwa wodini alikuwa anaongea na kuuliza mume wake yuko wapi, sasa nasikia siku iliyofuata ndipo akaanza kulalamika kuwa kifuani kinamuuma sana na hatimaye alifariki dunia.
“Dada ameacha watoto peke yao kwa kuwa walifanikiwa kupata watoto watatu,” alisimulia ndugu huyo kwa uchungu muda mfupi kabla ya kuanza safari ya kuelekea mkoani Songwe kwa ajili ya mazishi.
STORI: NEEMA ADRIAN, Wikienda