
MAMBO ni moto! Baada ya maneno kibao kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uhusiano wao, mchumba wa supastaa Wema Sepetu, Patrick Christopher ‘PCK’ kwa mara ya kwanza ameibuka na kutangaza ndoa, Risasi Mchanganyiko linakuwa la kwanza kukupa habari kamili.
Chanzo makini kililieleza gazeti hili kuwa kwa sasa Wema na PCK ambaye pia msanii wa Bongo Fleva aliyeimba nyimbo za Nitazame Usoni na Sweet Baby, mahaba ni kama yote kwani wana mpango wa kufunga ndoa ndani ya mwezi huu hivyo wako nchini Burundi ambako mwanadada huyo ameenda kutambulishwa kwa ndugu wa mume wanaoishi humo.
“Yaani unaambiwa Wema amekolea kwa PCK, hasikii wala haambiwi kuhusiana na mwanaume huyo kwani anampenda sana na kila wakati wako pamoja na wamekuwa wakienda nchi mbalimbali kwa matembezi.
“Ndugu zake Wema hawaupendi kabisa huo uhusiano kwa sababu ya madai yanayosambaa kwamba huyo jamaa ni tapeli na wameshamkataza mara kibao lakini mrembo huyo hataki kusikia chochote, kweli ameamua sasa,” kilidai chanzo.
PCK ATANGAZA NDOA
Akizungumza kwenye mahojiano maalum na Risasi Mchanganyiko kwa mara ya kwanza tangu tetesi za uhusiano wao zisambae mitandaoni, PCK alisema yupo ‘serious’, anamuoa Wema na ndoa hiyo itafanyika ndani ya mwezi huu.
Risasi: Umesema unamuoa Wema mwezi huu, je umeshajitambulisha kwao?
PCK: Ndiyo, tayari nimeshajitambulisha kwao wananifahamu.
Risasi: Tunajua una mke ambaye anaishi Mombasa na mlifunga ndoa, inakuwaje unasema utamuoa Wema?
PCK: Unajua licha ya kwamba naitwa jina la Kikristo lakini mimi ni Muislam na dini yangu inaniruhusu kuoa hadi wanawake wanne.
Risasi: Vipi mkeo wa Mombasa ameridhia au mlishaachana?
PCK: No coment.
Risasi: Ndoa yako na Wema mtaifungia wapi?
PCK: Dar.
Risasi: Je, itakuwa ni ya siri au hadharani?
PCK: Itakuwa ya hadhara kwa sababu siwezi kufunga ndoa ya siri na mtu ninayempenda.
Risasi: Wema hivi karibuni alifuta picha zote mlizokuwa pamoja alizokuwa ameweka kwenye ukurasa wake wa Instagram na ikasemekana mmemwagana, hili likoje?
PCK: Sisi tuko pamoja na tunapendana, hizo picha mimi ndiye niliyemwambia Wema azifute kwa sababu maalum ambayo siwezi kuitaja.
Risasi: Kuna habari kwamba ni marufuku wewe kuingia nchini Tanzania kwa sababu ya utapeli, hili likoje?
PCK: Hilo la marufuku na skendo za utapeli sizijui kwa kweli.
Risasi: Kuna madai kwamba Wema alikamatwa kwa utapeli na chanzo kikubwa ni wewe, hili nalo unalizungumziaje?
PCK: Watu wamekuwa wakiongea uongo sana kwenye mitandao ya kijamii, mbona hatupo Tanzania! Jamani watu waongee ukweli.
Risasi: Mko nchi gani kwa sasa?
PCK: Tuko Brazil.
Risasi: Huko mmeenda kufanya nini?
PCK: Tumekuja kutembea tu na tukitoka huku ndiyo tunakuja kufunga ndoa.
WEMA ANASEMAJE?
Alipotafutwa Wema ili kuzungumzia kuhusu ndoa hiyo simu yake haikupatikana hewani, hata alipotafutwa kwa njia ya Mtandao wa WhatsApp meseji haikuonekana kumfikia kuashiria kwamba namba hiyo haikuwa hewani.
Siku kadhaa zilizopita Wema katika ukurasa wake wa Instagram aliweka picha ya kimahaba akiwa na PCK na kuandika ‘future husband’ ambapo mashabiki wake walimshushia maneno makali wakimkosoa kwamba inakuwaje ameamua kumpenda mwanaume huyo.