MALKIA wa Sinema za Kibongo, Wema Sepetu ametangaza kuachana na maisha ya mitandaoni ambayo yamekuwa yakimletea kushusha heshima ya jina lake na kusema sasa anafunga jalada la maisha yake ya utoto na kuomba radhi kwa Watanzania kutokana na kusambaa mitandaoni kwa picha zake na anayedaiwa kuwa bwana yake zisizokuwa na maadili.
“Ninaomba radhi kwa Serikali yangu kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Bodi ya Filamu, familia yangu, ndugu zangu, jamaa na marafiki na wote wanaonipenda na kunisapoti kwa moyo mmoja, mama yangu mzazi ambaye alikuwa anaumia zaidi, wadogo zangu na wote ambao wananitazama kama kioo na kama mfano.
“Ninakiri nimewadharirisha wengi, nimewafedhehesha na nimewaathiri. Sipo hapa kwa ajili ya ku-justify wala kutoa sababu ya kile nilichokifanya maana haitabadilisha kitu. Sihitaji kumlamu mtu kwa hili, siombi radhi kwa kutafuta huruma ya mtu yeyote bali kwa kukiri nilichokifanya ni kibaya na ni zaidi ya aibu.
“Ninaomba radhi kwa waliokwazika na upuuzi niyoufanya, ninaweza nisieleweke kutokana na historia niliyo nayo, tangu nimeingia kwenye umaarufu mwaka 2006, nimefanya utoto na ujinga mwingi wa kuwavunja nguvu watu wengi walio nyuma yangu, lakini kuna mwisho wa kila kitu.
“Leo nasema kwa mdomo wangu nafunga jalada la utoto, ujinga, upuuzi na kila aina ya maumivu niliyosababisha kwa wtu wangu, naomba radhi kwa hili lililotokea na, namuomba Mungu aniongoze kwa amiasha yangu mapya kwa kuwa ndiye muweza wa yote, ASANTE,” amesema Wema.
Jana kupitia mitandao ya kijamii, zilisambaa video za mwanadada huyo akiwa na mwanaume aliyedai kuwa ni mume wake mtarajiwa ambaye alimpost siku za hivi karibuni katika ukurasa wake wa instagram.