
DAR ES SALAAM: Kama ulibahatika kuziona picha za staa wa filamu Bongo, Aunt Ezekiel akiponda raha nchini Dubai kusherehekea siku yake ya kuzaliwa na kujiuliza atakuwa ameteketeza shilingi ngapi, usipate tabu, Risasi Mchanganyiko limefanya naye mahojiano kwa kirefu.
Kwenye bata hilo, Aunt hakwenda peke yake, aliambatana na mwanaye Cookie pamoja na ndugu zake watatu ambapo wameonekana wakiponda raha katika viwanja mbalimbali nchini humo. Akizungumza na Risasi Mchanganyiko kwa njia ya simu kutoka Dubai, Aunt alianza kwa kusema kuwa, ameamua kufanya sherehe hiyo ya kuzaliwa nje ya nchi ikiwa ni moja ya kufurahia kutimiza miaka 30 akiwa tayari na mtoto wake.

“Nilipenda hii iwe ya tofauti kidogo na nilihitaji kufurahi na familia pekee ndiyo maana niliondoka na vijana wangu wawili na mdogo wangu pamoja na mtoto wangu kwa kweli nimeifurahia sana,” alisema Aunt. Akizungumzia gharama alizotumia, Aunt alisema kuwa, nauli za watu wanne pamoja na mtoto wake Cookie inakaribia shilingi milioni tano, gharama za hoteli ni shilingi milioni nne na ushee.
Kuhusu sherehe hiyo kwa maana ya vyakula na vinywaji, alisema haikuwa kubwa sana ambapo ilimgharimu takriban shilingi milioni 2. “Kuna wakati unajiuliza unafanya kazi kubwa sana lakini huna muda wa kupumzika hivyo unaweza ukajikusanya hata mwaka mzima kwa ajili ya kufurahi na familia yako na ndicho nilichofanya,” alisema Aunt.

Kuhusu kutokwenda kula bata hilo na mzazi mwenziye Moses Iyobo ‘Moze Iyobo’ alisema kuwa ilitokana na muingiliano wa majukumu ya kikazi na hana tatizo na Iyobo. “Watu wanasema sana kuona nimeenda peke yangu bila Iyobo lakini mbona inawezekana kabisa kitu hicho maana bado kuna vitu vingi tutakuwa pamoja tu,” alisema Aunt.
Hadi Risasi Mchanganyiko linakwenda mitamboni, Aunt alikuwa angali nchini humo akiendelea kufanya ‘shopping’ za hapa na pale kabla ya kurejea Bongo.
Stori:IMELDA MTEMA, RISASI MCHANGANYIKO