×

JPM Akataa Kutenga Fedha ya Katiba ya Warioba – Video

RAIS John Magufuli amesema kwa sasa hawezi kutenga fedha kwa ajili ya mchakato wa katiba mpya iliyopendekezwa na Tume ya Jaji Mstaafu, Joseph Warioba,  licha ya kutambua kiu ya wananchi kupata katiba mpya.

Magufuli ameyasema hayo leo Alhamisi, Novemba 1, 2018, wakati akizungumza kwenye Kongamano la Uchumi na Siasa lililofanyikia Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) na kusema kwa sasa kazi iliyoko mbele yake ni kuchapa kazi ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), miundombinu ya barabara, umeme, madawa na kuboresha huduma za kijamii.

 

“Watu kama Jaji Warioba wamefanya kazi nzuri, hata katiba mpya huwa sipendi kuizungumzia kwa sababu sikuinadi kwenye kampeni. Najiuliza tuanzie wapi kwenye rasimu ya Wairoba au ya Bunge? Ndiyo maana naona tuchape kazi kuliko kwenda kutumia fedha kuwaweka watu bungeni

 

“Lakini watu wameng’ang’ania katiba mpya utadhani ndiyo suluhisho la matatizo yote,” amesema Magufuli na kusisitiza kuwa hawazuii wanaotoa maoni yao, lakini mtazamo wake ni Tanzania kwanza. Kama kuna watu wanataka kuufadhili mchakato wa katiba mpya bora watupe tukajenge Stiegler’s Gorge na SGR,” alisema.

 

Mchakato wa katiba mpya ulizinduliwa na rais mstaafu, Jakaya Kikwete,  mwishoni mwa mwaka 2011 alipounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Mstaafu, Joseph Warioba. Mchakato huo uliishia kwenye Bunge Maalum la Katiba ambalo licha ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa haikupigiwa kura ya maoni hadi leo.

Rais Magufuli Kwenye Kongamano la Uchumi na Siasa Nchini – UDSM