KIPA wa zamani wa Yanga na Timu ya Taifa ya Tanzania, Peter Manyika amefunguka kuwa kipa Klaus Kindoki hana sifa ya kuidakia Yanga kwani ana uwezo mdogo.
Kindoki raia DR Congo juzi alifanya makosa yaliyosababisha Mwadui kupata bao la kusawazisha, ambapo wakati akijiandaa kuudaka mpira hafifu wa krosi uliopigwa na Charles Ilamfya ulimgonga kifuani kisha ukamtoka ambapo Salim Aiyee akauingiza kambani.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Manyika alisema Kindoki ambaye mpaka sasa amefungwa mabao manne katika mechi tatu alizodaka, hakuonyesha uwezo mzuri huku mabao mengi aliyofungwa yakitokana na uwezo wake mdogo.
Aliongeza kuwa, hata kama Kindoki akipewa mwaka mzima ili apandishe kiwango chake, itakuwa ni kazi bure kwa sababu hawezi kubadilika na sasa amefikia ukomo huku akiitaka Yanga kutafuta kipa mwingine mzawa.
“Kindoki hana sifa za kuichezea Yanga kwa sababu kiwango chake ni cha kawaida, Yanga waache tabia ya kuwaamini wachezaji kutoka nje kwa sababu yule Kindoki anaonekana ni mvivu wa mazoezi haiwezekani wenzake wacheze vizuri kuliko yeye wakati mwalimu wao ni mmoja tu, hafai kuichezea Yanga, hana kiwango hicho,” alifunguka Manyika.
Issa Liponda, Dar es Salaam