×

Wazungu waondoka na mafaili ya Salamba

TIMU tatu kutoka barani Ulaya ambazo zimeonyesha nia ya kutaka kumsaini mshambuliaji wa Simba, Adam Salamba, tayari zimepewa ‘makabrasha’ ya takwimu za mchezaji huyo kwa ajili ya kwenda kuzifanyia kazi.

 

Salamba ambaye tayari mambo yameanza kutiki kwenye kikosi cha Simba kwa kufanya vizuri kwenye ligi kuu akiwa amefunga mabao mawili, ameanza kunyatiwa na timu mbalimbali kutoka Ulaya.

 

Meneja wa Salamba, Jamal Kisongo ameliambia Championi Jumamosi kuwa, hadi sasa kuna timu tatu zimeleta ofa ya kumtaka Salamba ambapo zimehitaji takwimu zake kujua amecheza mechi ngapi msimu huu na ule uliopita na tayari wamefanya hivyo na kila kitu kinaweza kukamilika Desemba, mwaka huu.

 

“Kuna timu tatu ambazo zimeleta ofa za kumtaka Salamba moja kwa moja wakihitaji aende kufanya majaribio ambapo kwanza walihitaji takwimu zake kujua amecheza mechi ngapi msimu uliopita na msimu huu na idadi ya mabao aliyofunga, tayari tumeshakamilisha zoezi hilo kwa kuwasilisha video zake zote alizocheza.

 

“Kila kitu kimeshakamilika kwa upande wake lakini tunasubiri muda ufike ndio tujue anaende wapi, kwa sasa ni mapema mno kutaja timu hizo hadi mipango itakapokamilika ila nimeshaongea na mchezaji juu ya kujiandaa na safari,” alisema Kisongo.

Khadija Mngwai, Dar es Salaam