
YANGA jana walitua Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Mapinduzi Cup lakini nyuma ikiwaficha nyota wake akiwemo, Ibrahim Ajibu na Haruna Moshi ‘Boban’ jijini Dar.
Msafara huo ukiongozwa na kocha msaidizi, Noel Mwandila leo Alhamisi watacheza mechi yao ya kwanza dhidi ya KVZ huku mashabiki wakitarajia kuona maajabu ya wachezaji wengi
Vijana wa Yanga Yanga waliondoka huku wakiacha idadi kubwa ya mastaa wao jijini Dar es Salaam ikiwa ni mipango ya Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera ambaye amesema amezipumsha silaha zake kwa ajili ya ligi kuu Bara na michuano ya SportPesa.
Msafara huo wa Yanga uliondoka huku ukiwa na sura nyingi za vijana wa kikosi cha pili (B) pamoja na kocha wao Said Maulid ‘SMG’ ambaye ndiye atasaidiana na Mwandila katika kombe hilo ambalo Zahera halipi umuhimu.
Akizungumza na Spoti Xtra, Mwandila anasema: “Tunaenda huko kwenye Kombe la Mapinduzi lakini lengo letu ni kufanya vizuri katika kila mchezo wetu tukianza dhidi ya KVZ, licha ya kufahamu kuwa itakuwa mechi ngumu.
Kuhusiana na kuwaacha nyota wale wakubwa ni mpango wa mwalimu Zahera na alishasema juu ya hilo.” “Tutaenda kufanya vizuri na kikubwa tunataka mashabiki wetu watupe sapoti ileile kama ya mwaka jana 2018, tunawahitaji wao kutusapoti sisi,” alisema Mwandila raia wa Zambia.
Mechi hiyo ya Yanga itapigwa usiku wa leo kwenye Uwanja wa Amaan na kuonyeshwa moja kwa moja na Azam Tv. Yanga iliondoka na baadhi ya nyota wake wakiwemo; Deus Kaseke, Juma Mahadhi, Mwinyi Haji, Matheo Anthony, Juma Abdul, Jaffary Mohammed, Paul Godfrey ‘Boxer’, Ibrahim Hamad na wachezaji wengine wa timu B.