WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ametengua uteuzi wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Hamduni na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula, kwa kushindwa kutekeleza maagizo aliyoyatoa ya kupambana na rushwa ndani ya jeshi la polisi na kushindwa kutimiza wajibu wao.

Lugola ametangaza maamuzi hayo leo Jumatano, Januari 16, 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Pia ametengua uteuzi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhan Ng’anzi, kwa kumchukulia hatua askari mzalendo aliyetoa taarifa kuhusu magendo ya biashara haramu ya bangi na mirungi mkoani humo.

Vilevile, waziri huyo amemtaka Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama wa Bararabani, Fortunatus Muslimu, kujitathmini, kujitafakari na kujipima kama anatosha katika nafasi yake kutokana na vitendo ambavyo amevitaja kuwa askari wa usalama barabarani wamekuwa na tabia ya kuwakamata madereva wa bodaboda bila kufuata taratibu, kanuni na sheria.
Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu, ameagizwa kuunda tume itakayofanya kazi miezi mitatu kuchunguza vitendo na mianya ya rushwa katika kikosi cha usalama barabarani.
JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO
