×

SHIGONGO: Tusilalamike, Hatupo Hapa kwa Bahati Mbaya – VIDEO

MHAMASISHAJI maarufu Afrika Mashariki na Kati ambaye pia ni mjasiriamali, Eric Shigongo,  amewaasa vijana nchini kuacha kasumba ya kulaumu serikali na viongozi badala yake kuwa wazalendo, waipende nchi yao, wapambane kwa kufanya kazi kwa bidii, waishi katika ndoto zao na mwisho wa siku watafanikiwa.

 

Shigongo amesema hayo leo Januari 25, 2019 wakati akihutubia  kongamano lililoandaliwa na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kujadili changamoto zinazozikabili asasi za kiraia zinazoongozwa na vijana hapa nchini.  Kongamano hilo limefanyika  katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

“Vijana tunatakiwa kuwa na upendo kwa nchi yetu, hata kama kuna mambo yalifanyika kipindi cha nyuma na hatukufurahishwa nayo, hatutakiwi kulalamika, tukumbuke kwamba sisi ni Watanzania, hatupo hapa kwa bahati mbaya.  Ni mapenzi ya Mungu ndiyo yametuweka hapa, tuitetee nchi yetu, tuungane pamoja kwa kushirikiana, siku moja tutaondokana na umaskini,” alisema.

 

Alisisitiza kwamba mtu wa kwanza kumwiga na kufuatia utendaji wake wa kazi au shughuli yoyote, ni  baba mzazi ambapo iwapo akishindwa, mtoto hatakiwi kukata tamaa kwani akiwa na dhamira atapambana na kufanikiwa.

Alisema mafanikio huwa hayajali historia au ukoo fulani bali huja kwa mtu yeyote ambaye anaweza akawa kiongozi au tajiri mkubwa na jamii ikamkumbuka  maisha yote.

 

“Mazingira yasikukatishe tamaa, kama ulizaliwa na mwanamke, ukawa katika nchi hii, una nafasi ya kufanya makubwa na kuacha historia katika nchi hii. Binafsi huwa ninasema ukweli wangu kuhusu historia ya maisha yangu, sikuwahi kufaulu zaidi ya alama 25 darasani, na mtihani wa darasa la saba nilishindwa, niliposhindwa mtihani sikulia kwa sababu nilikuwa najijua, nilirudia nikashindwa,” Shgongo alisema akiweka bayana kwamba alirudia mara kadhaa akashindwa lakini kwa kuamini ndoto zake, alijikita katika biashara na kufika alipo leo.

Akifafanua njia aliyopitia, alisema kwamba alikuwa hajiamini na kwamba hata babu yake angefufuka leo angekufa tena kwa mshangao wa mafanikio aliyoyapata.

 

“Nilikuwa sijiamini kabisa, hata babu yangu akifufuka leo atakufa tena kwa sababu hataamni kama Shigongo mimi ndiye nilivyo leo, siyo kwamba sikuwa na akili, nilikuwa nazo lakini mfumo ndiyo unanifanya nijione mjinga, lakini leo nipo chuo kikuu,” aliwaambia wasikilizaji wake waliokuwa wanamsikiliza kwa makini akiwasihi watafute matatizo yaliyopo kwenye jamii na njia za kuyatatua kwani yatawapa fursa za kitu cha kufanya na kuwaingizia kipato.

VIDEO: MSIKIE SHIGONGO AKIZUNGUMZA HAPA