×

Jeneza Latelekezwa Likiwa na Mkungu Wa Ndizi – Video

Tukio lisilo la kawaida, limezua kizaazaa mkoani Arusha baada ya wakazi wa Mtaa wa Bondeni, Kata ya Endaseni wilayani Arumeru, kukuta jeneza likiwa limetelekezwa katikati ya shamba lililopo katika eneo hilo, tukio lililohusishwa na imani za kishirikina.

 

Baada ya kuliona jeneza hilo alfajiri ya leo, Septemba 22, 2021, wakazi wa eneo hilo wakiwa na taharuki, walikusanyika huku kila mmoja akiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichotokea, ambapo baada ya kulifungua, ndani yake kulikutwa mkungu wa ndizi ambazo hazijakomaa.

 

Juu ya jeneza hilo, pia kulikutwa msalaba ulioandikwa maandishi ya ajabu, yaliyosomeka ‘Born 1-100’ ambayo haikufahamika yalimaanisha nini.

 

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, baada ya majirani kukusanyika, walikubaliana kupiga simu kituo cha polisi ambapo muda mfupi baadaye, askari waliokuwa kwenye gari waliwasili katika eneo hilo.

 

Madai kutoka kwa mashuhuda ambayo hayajathibitishwa na Jeshi la Polisi, yanaeleza kuwa askari hao walipojaribu kulichukua jeneza hilo, ilishindikana na muda mfupi baadaye, gari walilokuja nalo lilipata hitilafu na baada ya kutengenezwa, askari hao waliondoka na kuliacha jeneza hilo.

 

Baadaye, mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mtumishi wa Mungu, alifika eneo hilo na baada ya kukubaliana na mmiliki wa shamba hilo ambayo hakutaka kujitambulisha jina lake, walikubaliana kulichoma jeneza hilo.

 

Muda mfupi baadaye, jeneza hilo lilichomwa moto pamoja na mkungu wa ndizi uliokuwa ndani yake na kuacha gumzo kubwa kwenye eneo hilo.

 

 

Leave a Comment