×

SIMANZI NJOMBE! MAZISHI YA WATOTO 3 WA FAMILIA MOJA WALIOUAWA

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, akizungumza na wananchi waliohudhuria mazishi ya watoto watatu wa familia moja waliouawa kikatili katika kijiji cha Ikando Kata ya Kichiwa, wilayani Njombe, ambapo aliahidi serikali kukomesha mauaji hayo.

HALI ya majonzi, vilio na simanzi ilitawala katika kijiji cha Ikando Kata ya Kichiwa, wakati wa mazishi ya miili ya watoto watatu wa familia moja waliouawa kikatili ikiwa takribani mwezi mmoja sasa tangu matukio ya kupotea na kuuawa kwa watoto mkoani Njombe.

 

Akizungumza katika mazishi ya watoto hao watatu; Godliver Mwenda (11), Gasper Nziku (8) na Geribet Nziku (5), Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni,  amesema serikali inalaani mauaji hayo na imejipanga kuhakikisha inadhibiti na kutokomeza mtandao huo unaojihusisha na mauaji hayo ya kikatili kwa watoto.

Masauni akiweka mchanga katika moja ya makaburi ya watoto hao.

 

“Tukio hili halitopita burebure na tunataka iwe fundisho kwa watu wengine wote wenye roho za kinyama waliotekeleza mauaji haya na tayari baadhi ya watuhumiwa wa mauaji haya tayari wameshakamatwa kupitia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama likwemo jeshi la polisi,” alisema Masauni.

 

“…Nataka nitoe ujumbe huu kwa nchi nzima kwamba mtu yoyote ambaye anajishughulisha na mauaji dhidi ya binadamu wakiwemo watoto wadogo kama hawa tunamhakikishia tutamkamata na serikali haitolala katika hili,” aliongeza Masauni.

Moja ya majeneza  hayo likiingizwa kaburini.

 

Akizungumza wakati wa mazishi hayo baba wa marehemu hao, Danford Nziku, ameiomba serikali kuimarisha ulinzi maeneo mbalimbali katika kijiji hicho huku akisisitiza kutafutwa kwa watuhumiwa waliohusika na mauaji ya watoto wake.

 

“Watoto wangu wameondoka wakiwa bado na umri mdogo sana, ndoto zao sasa zimezimwa ghafla baada ya kufanyiwa ukatili, na wao si wa kwanza kufanyiwa matukio hayo ndani ya mwezi huu, naiomba serikali yangu kuimarisha ulinzi katika maeneo haya, sasa naishi kwa hofu hapa nyumbani na mke wangu,” alisema Nziku.

 

Ndugu wa familia iliyopoteza watoto watatu wakiweka kaburini nguo za mmoja wa watoto hao ikiwa ni utekelezaji wa mila na desturi ambapo marehemu huzikwa na nguo zake zote.  

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake,  mkazi wa Kijiji cha Ikando amesema matukio hayo yametokea sana kipindi cha nyuma huku akiiomba serikali kupiga vita ramli chonganishi kupitia uhalali wa waganga wa kienyeji waliopo wilayani humo.

 

“Vifo hivi vinasikitisha sana  nadhani serikali iandae utaratibu wa kuwahakiki hawa wataalamu wetu wa kienyeji, wamekuwa chanzo cha malumbano mengi hapa kijijini.  Watu wamekuwa wakituhumiana mambo ya uchawi, hali inayopelekea kuwepo kwa visasi kati yao ambavyo hupelekea vifo kama hivi,” alisema mwananchi huyo

Waombolezaji wakiwa wamebeba majeneza ya watoto Godliver Mwenda, Gasper Nziku na Geribet Nziku.

 

Akizungumzia mauaji hayo,  Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kibena, Barnabas Baraka,  amesema vifo vya watoto hao vimetokana na kushambuliwa na vitu vizito na vyenye kali maeneo ya kichwani huku mmoja kati ya maiti hizo akiwa amekatwa sikio la kulia.

VIDEO: RAIS MAGUFULI AWAPA MAAGIZO MAZITO VIONGOZI WAPYA