×

Simba Yashusha Kocha Mpya

Kocha Msaidizi, Etienne Ndayiragije raia wa Burundi.

SIMBA haitaki utani kwani imezidi kuliimarisha benchi lake la ufundi, sasa imeamua kumshusha Kocha Msaidizi, Etienne Ndayiragije raia wa Burundi ambaye kama mambo yatakuwa sawa atakuwa kwenye benchi Jumanne dhidi ya Al Ahly.

 

Simba haijawa na kocha msaidizi tangu alipoondoka Masoud Djuma Oktoba mwaka jana kutokana na kushindwa kuelewana na Kocha Mkuu, Mbelgiji Patrick Aussems na sasa ina michuano migumu ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.

 

Taarifa ambazo Championi Jumamosi limezipata zinasema kuwa, uongozi wa Simba upo kwenye mazungumzo ya mwishomwisho na Ndayiragije ili akawe msaidizi wa Aussems.

 

Inadaiwa kuwa uamuzi huo ulifikiwa hivi karibuni katika kikao cha Bodi ya Wakurugenzi ya Simba kilichofanyika juzi jijini Dar na kuongozwa na mwekezaji mkuu wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’.

 

Habari za kuaminika zinasema viongozi hao kwa pamoja walikubaliana na hilo kutokana na kuridhishwa na uwezo wa Ndayiragije tangu alipotua hapa nchini na kujiunga na Mbao FC na sasa amekuwa akiiongoza vyema KMC kwenye ligi.

 

Mpaka sasa KMC ambayo imepanda daraja msimu huu imekuwa ikionyesha soka la kuvutia na sasa ipo nafasi ya tano kwenye ligi ikiwa na pointi 35 baada ya kucheza michezo 24 na kuzipiku klabu kongwe ikiwemo Prisons.

 

“Jambo jingine ambalo uongozi huo umeliona ni suala zima la mawasiliano, Aussems ana uwezo mkubwa wa kuzungumza Kingereza na Kifaransa ambayo ndiyo lugha yake mama lakini pia Ndayiragije naye anazijua vizuri lugha zote hizo lakini pia faida nyingine kwake ni kwamba anaweza pia kuongea Kiswahili kwa ufasaha.

 

“Kwa hiyo, Aussems atakuwa amepata nafuu katika kuwasiliana na wachezaji hasa wale wasiojua vizuri Kingereza au Kifaransa ila wanajua Kiswahili pekee,” kilisema chanzo hicho cha habari na kuongeza kuwa:

 

“Uongozi unaendelea kufanya naye mazungumzo ili kuhakikisha unainasa saini yake mapema iwezekanavyo kabla ya timu hiyo kupambana na Al Ahly Jumanne ijayo hapa jijini Dar es Salaam.”

 

Alipoulizwa Katibu Mkuu wa Simba, Dr Arnold Kashembe kuhusiana na hilo alisema: “Mpango huo wa kutafuta kocha msaidizi upo na mazungumzo yanaendelea lakini kwa sasa sina cha kusema kwa sababu bado haujakamilika.”

 

Kwa upande wa KMC, ofisa habari wa timu hiyo, Anuary Binde akizungumzia ishu hiyo, alisema: “Kwa upande wetu hatujapata taarifa hizo kama uongozi kwa hiyo hatuna la kusema, lakini pia itambulike kuwa Ndayiragije bado tuna mkataba naye wa miaka miwili wa kufundisha timu yetu.”