×

Yanga Waifuata Kibabe Namungo

Kikosi cha timu ya Yanga

MSAFARA wa wachezaji 20 na Benchi la Ufundi la timu hiyo likiongozwa na Kocha Mkuu wa Yanga Mkongomani, Mwinyi Zahera, leo alfajiri umesafiri kuelekea Ruhangwa, Lindi kwenda kuvaana na Namungo FC.

 

Yanga, keshokutwa Jumapili jioni inatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Majaliwa mjini huko kwa ajili ya mchezo huo wa Kombe la FA.

 

Timu hiyo, inaelekea Ruhangwa kucheza na Namungo ikiwa ni siku moja tangu itoke kucheza mchezo wake wa Ligi Kuu Bara na Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ambao ulimalizika kwa Yanga kushinda mabao 2-1.

Akizungumza na Championi Ijumaa, mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema kuwa timu yao ilirejea jana alfajiri ikitokea Mwanza kwa ndege ya Air Tanzania kabla ya leo alfajiri kuanza safari ya kuelekea Ruhangwa kwa ajili ya mchezo huo.

Alisema katika msafara huo wataongezeka wachezaji wawili ambao hawakuwepo Mwanza kwa ajili ya mchezo dhidi ya Mbao FC ambao ni Feisal Salim ‘Fei Toto’ na Gadiel Michael waliokuwa wanatumikia adhabu ya kadi tatu za njano walizozipata katika michezo iliyopita ya ligi.

 

“Maandalizi ya timu yetu yanaendelea vizuri na kikosi kipo fiti kwa ajili ya mchezo wetu huo wa FA, tunafahamu ratiba inatubana, lakini tutajitahidi kuhakikisha tunapata ushindi.

 

“Tunatarajia kusafiri kesho (leo) asubuhi kwa basi letu tunalolitumia kuelekea Ruhangwa tayari kuwakabili wapinzani wetu Namungo, tuna kibarua kigumu katika mchezo huo lakini hatuna hofu tutapata ushindi kutokana na ubora wa timu yetu,” alisema Saleh.