
Nyota Waziri ni mmoja wa wanamuziki wa kike wakubwa nchini ambaye alianza kufahamika kupitia Kilimanjaro Band ‘Njenje’ aliyoanza nayo tangu 1989.
Nyota amekuwa mwiba kwenye bendi hiyo kupitia vibao vikali kama vile Gere, Tulizana na vingine vingi na ni mwanamke pekee aliyekuwepo kwenye bendi hiyo.
Over Ze Weekend limemtafuta na kufanya naye mahojiano exclusive kwenye safari yake ya muziki alipotoka hadi sasa;
Over Ze Weekend: Kumekuwa na ukimya mkubwa sana kwenye bendi ya Njenje tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, nini kilichotokea?
Nyota: Njenje ipo kama kawaida lakini tulipumzika kidogo na muda si mrefu tutarudi tena.
Over Ze Weekend: Lakini mnaposimama kwa muda kutofanya kazi huoni kama mnawapoteza mashabiki wengi?

Nyota: Unajua mashabiki wa Njenje wapo siku zote, mwanzo tulikuwa tunapiga pale Palm Beach, lakini kwa sasa tunasubiri pale Makumbusho pakamilike kwanza tutahamia hapo na mashabiki wetu watajua.
Over Ze Weekend: Kufunga bendi mwisho saa sita imewahi kuwaathiri?
Nyota: Ndiyo! Unajua ile kufunga mabendi saa sita ilitugharimu sana, mashabiki wengi wakawa hawatoki kabisa, lakini kwa vile sisi tulikuwa tukifanya kazi kwa malengo hivyo haikutusumbua sana.
Over Ze Weekend: Umekaa muda mrefu sana ndani ya bendi ya Njenje, nini siri ya kutohamahama kama wanamuziki wengine?
Nyota: Sisi Njenje tunaishi kama ndugu, yaani kila kitu unachofanya unajua na wewe una shea yako yaani kila mtu bendi ni yake hivyo kama uko tayari kuona kitu chako kinapotea ndiyo unaweza kuhama lakini vinginevyo ni mpaka mwisho.
Over Ze Weekend: Zaidi ya kuimba ni kitu gani kingine unafanya?
Nyota: Mimi ni mfundaji wa maharusi lakini ni mshehereshaji (MC) mzuri tu kwenye maharusi mbalimbali kwa hapo namshukuru sana Mungu ananipa riziki pia.
Over Ze Weekend: Bendi ya Njenje ilitokea kupendwa sana, nini siri yake?
Nyota: Unajua ni kwamba wanamuziki wenyewe wa bendi tuliishi kindugu na kupendana sana hivyo tukawatengenezea mpaka mashabiki zetu kupendana pia.
Over Ze Weekend: Nakushuru sana kwa ushirikiano wako
Nyota: Karibu sana!
IMELDA MTEMA