
Rais Dkt. John Magufuli amekata utepe kuashiria ufunguzi wa Barabara ya Namtumbo-Tunduru, mkoani Ruvuma ambako amekwenda kwa ziara ya kikazi ya siku tano kuanzia leo Aprili 5, 2019..
Nilijua mkutano wa ufunguzi ungefanyika Mjini badala ya kuwasumbua wananchi kutembea, lakini hiyo ndiyo mipango ya watu ambao si wanasiasa, mwanasiasa angepanga Mkutano mjini, na mimi nilitaka niuone vizuri Mji wa Tunduru.
Nilipita kuwaomba kura 2015, niliwaombea Madiwani na Wabunge na hapa Tunduru kulikuwa na upinzani mkubwa sana, lakini kwa Moyo wa upendo mkanipa mimi mtumishi wenu ambaye nilikuwa sistahili cheo hichi.
Sio kwamba Tanzania yote ina lami, mnapopata kitu fulani mnataka kila kitu kiwekwe huko, Waziri wa Ujenzi yupo hapa anatokea Mkoa wa Katavi Mji wa Mpanda Jimbo lake halina lami, japo yeye anasimamia kujenga lami lakini kwake hakuna lami. Ndugu zangu wa Tunduru tuwe na picha ya ukweli, kwamba Serikali imebeba mzigo kuhakikisha barabara inatengenezwa, tunataka tufungue Ukanda huu, wananchu usipowapelekea barabara umewacheleweshea maendeleo.
Na kwa sababu hii tusiwe wa kuwasahau wengine tukaanza kuomba lami kila barabara, wakati uwezo huo kama nchi bado hatujafikia hapo. Hata kuwa na Mikoa yote hii ishirini na kitu kwa mawazo yangu mafupi hapakuwa na sababu, tungeweza kuwa na Mikoa michache zile gharama za kuendeshea tungezipeleka kwa maslahi ya wananchi, tukajenga hospitali na wakawa na magari ya wagonjwa.
Tunazungumzia nchi ya viwanda lakini viwanda vimelala, ni lazima watendaji wangu mbadilike, ukipewa Wizara ya Viwanda lazima ushughulikie viwanda, kweli Naibu Waziri ushughulikie vya Dar es Salaam wakati vya Mkoa wako bado.
Huku washtakiwa wengi wanaua Tembo wetu, wakiua Tembo kule wanawaleta huku wakiua huku wanawapeleka kule mtandao wote tushaujua mkae mwendo wa mchakamchaka, wako wengine wanashirikiana na viongozi.
Endeleeni kuwaombea viongozi wenu, wakaishike dhana ya utumishi badala wao kutumikiwa, wakaelewe cheo ni dhamana na watambue vyeo wamepewa na Mungu, wakitumia vibaya watambue siku moja watajibu mbele ya haki.
Barabara hii tangu tupate uhuru, Watu walikuwa hawadhani kama Watu wa Tunduru watapita kwenye lami. Inawezekana hata huko wazee wetu walipo ukiwaambia Tunduru kuna libarabara ligumu, hawatakuelewa.
Naijua Tunduru na maeneo yote tangu nikiwa Waziri. Nimehangaika kwenye barabara hii na wapo niliowaudhi. Wananchi niliowabomolea nyumba zao na wengine, naomba wote mnisamehe. Mwingine niliyemuudhi ni yule Mkandarasi anaitwa Progress tuliyempa sehemu zote tatu awali. Alipewa akaweka vifaa bila kufanya kazi, nikamchongea kwa mzee Mkapa tukamfukuza na vifaa vyake tukapiga mnada. Hii ndio sheria.
Wahandisi ambao wamekuwa wakifanya vibaya ni Waandisi wa Maji, tangu enzi za Kamwelwe, nilikupeleka pale nikadhani utabadilisha. Miradi mingi ya maji haikamiliki, na kuna miradi mingi ya maji hewa, ukifungua hakuna maji yanatoka
Naona mliomba mnataka Tunduru iwe Mkoa lakini ndugu zangu bado. Maendeleo si kufanya uwe mkoa ila wapelekee vitu muhimu. Watu wa Tunduru hawataki kumuona Mkuu wa Mkoa na kitambi chake. Wanataka maendeleo, hospitali, shule na vingine. Mimi kwa akili zangu hizi, mikoa 26 hii tungepunguza iwe michache tuihudumie vizuri. Mmeanza kujenga hospitali ya Wilaya na mambo bado hayajawa vizuri. Sasa nawaongezea Milioni 200. Siwezi kutoa fedha eti najenga ofisi ya RC Tunduru,” amesema Maagufuli.