×

Simba Sc hamna sababu ya kuiacha Mazembe leo

NI siku nyingine ambayo Simba wanakabiliwa na mchezo mgumu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo kwa sasa timu hiyo ipo hatua ya robo fainali.

 

Simba leo Jumamosi itakuwa na mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam dhidi ya mabingwa mara tano wa michuano hiyo, TP Mazembe kutoka DR Congo.

 

Mchezo huo ni mwendelezo wa michuano hiyo msimu huu ambapo Simba tangu imeanza imeweza kushinda mechi zake zote ilizocheza nyumbani. Ilianza kwa kuifunga Mbabane Swallows ya Eswatini mabao 4-1, ikaichapa Nkana 3-1.

 

Hiyo ni katika hatua ya awali na ya kwanza. Kwenye makundi, ikazifunga JS Saoura 3-0, Al Ahly ikafungwa 1-0, kisha AS Vita Club nayo ikachapwa 2-1.

 

Hapo ndipo safari ya Simba kutinga hatua ya robo fainali ikawa imeenda hivyo. Kama ujuavyo, malengo ya Simba kwa msimu huu yalikuwa ni kufika hatua ya makundi, ilipofika makundi, kocha wa kikosi hicho, Patrick Aussems, akaweka mikakati ya kushinda mechi za nyumbani zote. Mkakati huo ukafanikiwa kwa asilimia zote.

 

Ukitazama Simba iliposhinda nyumbani mechi zote tatu, ikafungwa zote za ugenini. Lakini kikubwa ni kwamba imesonga mbele kutokana na malengo na hesabu zao kwenda sawa. Hivi sasa ipo kwenye hatua ya robo fainali ambayo ina mechi mbili pekee.

 

Nyumbani na ugenini. Simba inaanzia nyumbani ambapo kwa rekodi zao ikicheza hapo, ni wazi kuna uwezekano wa kushinda leo. Licha ya hivyo, lakini Simba inatakiwa kutotembelea nyota hiyo zaidi ya kujipanga kusaka ushindi kwa sababu TP Mazembe nao wanalifahamu hilo, ni wazi watakuwa wamekuja kwa kusaka ushindi au hata wakipata sare kwao ni nafuu sana.

 

Katika mechi hizi za ugenini na nyumbani, ukiruhusu nyumbani kwako kupoteza hata pointi moja basi ni ngumu kutusua ugenini kwa sababu soka lina mambo mengi sana. Kuna fitina za wazi zinafanywa na timu nyingi zinapokuwa nyumbani kwao katika kuhakikisha zinafanikisha malengo yao ya kuibuka na ushindi.

 

Zinatambua kwamba nazo zikiwa ugenini zitafanyiwa michezo hiyo mibaya. TP Mazembe tunafahamu ni timu kubwa na yenye wachezaji pengine wa hali ya juu kuliko wale wa Simba. Nimemsikia nahodha wa kikosi hicho, Rainford Kalaba akisema kwamba leo atakutana na Simba kwa mara ya tatu akimaanisha kwamba mwaka 2011 alikutana nayo kwenye zile mechi mbili za nyumbani na ugenini, na leo ni ya tatu.

 

Kalaba anasema Simba ile ya mwaka 2011 ilikuwa na staa mmoja pekee ambaye ni Mbwana Samatta, lakini hivi sasa wapo wengi na Simba hii inaweza kuwa kikwazo kwao. Nikukumbushe kidogo kwamba, mwaka 2011, Simba ilifungwa 3-2 hapa nyumbani, ugenini ikafungwa 3-1. Kama hata wao wenyewe wanalitambua hilo, ni jukumu la wachezaji wa Simba sasa kudhihirisha ubora wao kwa kuibuka na ushindi leo na si kitu kingine. Kama Simba leo itashindwa kuwapa raha Watanzania kwa kuibuka na ushindi, kuna hatari zaidi mechi ya marudiano.

 

Simba hakikisheni mnashinda mechi ya leo ili iwe rahisi mechi ya marudiano ambapo mkienda kwao, wenyeji wenu watakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha na wao wanashinda ili kuwaondoa. Ni wazi TP Mazembe wamekuja kuhakikisha hawapotezi mchezo wa leo, hivyo watakuwa wamejiandaa na mchezo wa marudiano kule kwao iwe isiwe waibuke na ushindi.

 

Sasa inatakiwa waondoke hapa wakiwa na mlima mrefu wa kupanda na hilo litatokea endapo tu wataacha pointi zote tatu hapa nyumbani. Mashabiki wa Simba na Watanzania kwa jumla, kama ilivyokuwa awali mlivyojitokeza kwa wingi uwanjani kutoa sapoti kwa timu yenu, iwe hivyo na leo ili kuwaongezea morali wachezaji. Uwepo wenu ni sehemu ya kuwafanya wachezaji kupambana zaidi kusaka ushindi kwa sababu watakuwa wakicheza wakitambua kwamba wana deni kubwa wanalotakiwa kulilipa kwenu. Ili deni hilo lionekane kubwa zaidi, mashabiki mkiwa uwanjani hakikisheni mnashangilia kwa nguvu zote mwanzo hadi mwisho wa mchezo. Hakuna kuacha kushangilia hata kitokee nini. Mwisho kabisa niwatakie kila la heri Simba katika mchezo wa leo. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Simba SC.