Mbunge wa Nzega (CCM), Hussein Bashe amesema eneo la kibiashara la Kariakoo jijini Dar es Salaam limekufa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kazi ya ukusanyaji kodi kufanywa na watu ambao hawajasomea fani hiyo.
Bashe ameyasema hayo jana wakati akichangia makadiro na mapato na matumizi ya ofisi ya waziri mkuu na mfuko wa bunge kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
“Lazima watu serikalini wafahamu suala la mtu kuchukua shilingi mia moja yake kwenda kuwekeza kwenye nchi fulani, namba moja inategemea mtazamo wake kwamba naenda kuweka pale iko salama. Leo Kariakoo is dead (imekufa),” alisema.
Bashe alimpongeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kwenda kuzungumza na wafanyabiashara wa Kariakoo lakini akaishauri Serikali kupeleka marekebisho ya sheria kama mpango wa kuboresha mazingira ya biashara (blue print).
Alisema pia kama suala hilo linahitaji uhamasishaji ndani ya Serikali basi lifanyike na kwamba Benki ya Dunia (WB) imetoa ripoti ya maeneo ambayo yanaisumbua Tanzania katika uwekezaji ikiwAmo utitiri wa kodi ndogo ndogo.
“Leo inaanzishwa task force. Eti ile task force ina polisi wanaenda kukusanya kodi. Polisi kasomea wapi ukusanyaji wa kodi? Takukuru kasomea wapi ukusanyaji wa kodi? ina watu kutoka idara nyeti za Serikali, ina watu wa TRA,” alisema.
Alisema kundi hilo linakaa Kariakoo ambapo mtu akitokea na mfuko wake wanamwambia karatasi ya ulipaji kodi kwa njia ya eletroniki ni feki.
“Huyu mtu katoka Congo anajuaje kama EFDs yake ni feki? Sikujua (anajibu), anachukuliwa anawekwa Msimbazi polisi next time (wakati mwingine) haji anaenda Uganda ama nchi nyingine, ”alisema.
“Ni lazima suala la ukusanyaji kodi liachwe kwa waliosomea ukusanyaji wa kodi. Polisi wakafanye kazi yao, Takukuru wakafanye kazi yao.”
Aidha, alisema lazima kuweka kilimo kama eneo muhimu la fungamanishi ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu.
Alitaja eneo la pili la kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu ni la masoko ambapo amesema imeanzishwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) lakini ina tatizo la kimuundo.
Alisema benki hiyo iko chini ya wizara ya fedha na mipango wakati bodi za mazao ziko chini ya wizara ya kilimo, suala la masoko liko chini ya wizara ya viwanda na biashara na suala la uwekezaji kwenye ofisi ya waziri mkuu.
“Ushauri wangu ni lazima kutafuta namna ya kufanya strategic alliance kati ya wizara zote kwenye suala la marketing ya mazao ya wakulima ili TADB iweze ku-finance bodi ya mazao mchanganyiko kama tunaenda kwenye msimu tuweze ku-plan nje kuna mahitaji ya kiasi gani na masoko yako wapi Serikali isihitaji ku-finance,” alisema.
Alisema bila kufanya hivyo hata vije viwanda vya magari na vingine vitakuwa havina uwezo wa kuzalisha kwa sababu watu watakuwa hawana uwezo wa manunuzi.