
WAKATI wapenzi na mashabiki wa soka hapa nchini wakitaka kujua hatima ya aliyekuwa kipa wa Yanga, Beno Kakolanya ya kutua Simba, mambo bado si shwari kwake baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kudaiwa kumwekea kauzibe juu ya kujiunga na timu hiyo.
TFF inadaiwa kukwamisha mpango huo wa Kakolanya kutua Simba, kutokana na kushindwa kulimaliza suala lake na uongozi wa Yanga kwa wakati, juu ya mkataba wake baada ya kutimuliwa kikosini hapo na kocha mkuu wa timu hiyo raia wa DR Congo, Mwinyi Zahera.
Zahera alimtimua Kakolanya katika kikosi cha Yanga wakati akiwa bado na mkataba mpaka mwaka 2020 kwa madai kuwa ni msaliti kutokana na kugoma kuitumia timu hiyo akishinikiza kulipwa madai yake.
Habari za kuaminika ambazo Championi Jumamosi limezipata zimedai kuwa kutokana na hali hiyo, Simba wameshindwa kumpatia mkataba wa kujiunga na timu hiyo mpaka suala lake litakapomalizika.
Hata hivyo, Meneja wa Kakolanya, Selemani Haroub, alipoulizwa kuhusiana na hilo, alisema kuwa mpaka sasa kipa huyo hajui msimu ujao atakuwa na timu gani kutokana na TFF kushindwa kulipatia ufumbuzi suala lake hilo na Yanga.
“Lakini kuhusu ishu ya Kakolanya kusaini Simba hilo siwezi kulizungumzia kwa sababu mpaka sasa suala lake na Yanga halijamalizika.
“Tulilipeleka TFF kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi lakini mpaka sasa bado, kama litapatiwa ufumbuzi basi hapo ndipo tutakuwa katika hatua nzuri ya kusema chochote,” alisema Haroub
Stori: SweetbertLukonge, Dar es Salaam