
DAR ES SALAAM: Maji hufuata mkondo, lakini safari hii mkondo ndiyo umefuata maji! Ndiyo hali halisi ya kinachojiri kwenye maisha ya baba mzazi wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul Jumaa ‘Diamond Platnumz’, Abdul Jumaa almaarufu Baba D.
SHOO MBILI TU, LAKINI….
Baada ya kupiga shoo mbili tu za nguvu, tayari Baba D anapitia maisha yaleyale aliyopitia mwanaye Diamond au Mondi wakati anashika kasi ya ustaa. Kama ilivyokuwa kwa Mondi yapata miaka 10 iliyopita alipokuwa akipata umaarufu kupitia muziki wa Bongo Fleva alivyokuwa akishobokewa na mademu, ndiyo hivyohivyo inavyotokea kwa baba yake sasa.
SHOO YA PASAKA
Achana na shoo ya jijini Dodoma wiki moja iliyopita ambapo Baba D alikuwa gumzo huku warembo wakitamani kumshika tu na kupiga naye picha, lakini gumzo ni shoo ya Sikukuu ya Pasaka aliyofanya kwenye Hoteli ya King D iliyopo Sinza-Afrika Sana jijini Dar. Katika shoo hiyo iliyoshuhudiwa na gazeti hili, Baba D aliangusha bonge la shoo iliyosababisha mashabiki wake kupagawa.

MREMBO AMGANDA
Mmoja wa mashabiki wake alikuwa mrembo mmoja mkali ambaye jina halikupatikana mara moja ambapo yeye alimganda Baba D kuanzia mwanzo wa tukio hilo hadi mwisho.
KABLA YA KUPANDA STEJINI
Kabla ya kupanda stejini, Baba D aligeuka sukari ya warembo kwani kila mmoja alitaka kuwa naye karibu, lakini huyo mmoja ndiye aliyeonekana kuwafunika wenzake na kuwa beneti na msanii huyo ambaye nyota yake inazidi kung’aa kila kukicha. Wakati Baba D akisubiria kupanda stejini, mrembo huyo alikuwa amekaba kuhakikisha hakuna mtu anamsogelea huku akimpetipeti na kumuonesha mahaba kama yote.
STEJINI SASA
Mishale ya saa 6:00 usiku, Baba D ndipo alipopanda stejini na kuangusha shoo ya kukata na shoka, lakini wakati akipagawisha mrembo huyo alishindwa kuvumilia na kumpandia stejini.
Akiwa stejini hapo, mrembo huyo alimkatia Baba D mauno ambayo siyo ya nchi hii hadi mzee huyo akatokwa na kijasho chembamba. Hata hivyo, baadaye mrembo huyo alitoa kitambaa kisha akawa anamfuta jasho hadi shoo ilipomalizika ambapo alishuka naye na kwenda kukaa naye pembeni kisha kuanza kumpepea.
BABA HAKUTEGEMEA
Akizungumza na Amani juu ya matukio hayo, Baba D aliwashukuru mashabiki wake wote na kwamba hakuamini kama wangejitokeza kwa wingi kiasi hicho. “Mimi ninawashukuru sana kwa namna ambavyo wamenipokea kwani sikutegemea. Nawaomba waendelee kuniunga mkono kwani ndiyo kwanza mimi ni mchanga kwenye gemu ila ninawaahidi kuwa sitawaangusha,” alisema Baba D akiahidi kufanya mazoezi ya pumzi ili kutochoka haraka wakati wa kuangusha shoo.

Alipoulizwa juu ya mrembo aliyekuwa amemganda, Baba D alikuwa na haya ya kusema; “Hii ndiyo hali inayotokea kila ninapokuwa, iwe kwenye shoo kama ilivyokuwa Dodoma, ilivyotokea hapa na pengine popote. “Hao ndiyo mashabiki wangu na mimi siwezi kuwafukuza kwani nitaonekana ninaringa. Najua nina mashabiki wengi, siyo warembo tu bali hata masela ni mashabiki wangu.”
Hadi shoo hiyo inamalizika majira ya saa 9:00 usiku, Baba D alikuwa hoi kutokana na kutozoea mazingira ya kukesha kwani ndiyo kwanza ameanza shoo za usiku hivyo alilazimika kuondoka ukumbini na kusepa zake huku akimwacha mrembo huyo ambaye naye aliondoka kivyake.
NYIMBO ZA BABA D
Tangu aingie rasmi kwenye gemu, tayari Baba D ameachia ngoma mbili, moja ikiwa na video yake inayokwenda kwa jina la Mwewe akishirikiana na msanii aitwaye Sungura na nyingine ni Unanijua ambayo bado video yake haijatoka ambayo amemshirikisha msanii anayefahamika kwa jina la Chada Boy.