The House of Favourite Newspapers

Yanga Yavuta Mkali wa Okwi

YANGA wametua kwa straika mzawa mwenye mabao sawa na Heritier Makambo anayeondoka Jangwani. Lakini kilichowanogea ni kwamba huyo jamaa ambae ni Salum Aiyee wa Mwadui anawazidi kwa mabao wakali wawili ambao Simba inawaaminia kwelikweli. Yaani Emmanuel Okwi na John Bocco.

 

Aiyee mwenye miaka 25, ametupia mabao 16 msimu huu sawa na Makambo huku Meddie Kagere wa Simba mwenye 20 akiongoza safu ya wafungaji katika Ligi hiyo ambayo mpaka sasa bingwa hajui atapewa nini. Okwi na Bocco wote wana mabao 15 kila mmoja na timu yao inacheza leo Jumapili na Ndanda kwenye Uwanja wa Uhuru ambao nyasi zake bandia ziliwekwa hivi karibuni na CAF.

 

Habari za ndani ya Yanga ambazo Spoti Xtra imezipata ni kwamba Mwinyi Zahera na baadhi ya vigogo wa Yanga wameamua kumpa kipaumbele Aiyee miongoni mwa wachezaji wazawa kutokana na kiwango chake cha msimu huu. Habari zinasema kwamba Yanga wamezungumza nae wiki iliyopita na alipoulizwa na Spoti Xtra alikiri kwamba kuna kitu kinaendelea na muda wowote anaweza kupokea simu nyingine ya kuitwa Dar es Salaam kumaliza dili.

 

“Siwezi kumtaja jina lakini tulizungumza mambo mengi ikiwa ni pamoja na mkataba wangu wa Mwadui FC ambao alitaka kujua unamalizika lini.

 

“Nilimwambia kuwa Mkataba wangu unamalizika hivi karibuni baada ya ligi kufikia ukingoni, nilikuwa na mkataba wa mwaka mmoja tu,akaniambia hofu yao walijua nina mkataba mrefu,”alisema Aiyee ambae ana weusi wa asili.

 

“Kuhusiana na ishu ya kujiunga na Yanga nilimwambia kuwa mimi sina tatizo sababu soka ndiyo biashara yangu kama watanipa dau zuri ambalo nitakubaliana nalo basi sina tatizo,”alisema Aiyee ambaye timu yake ikifungwa na Lyon Jumatano mjini Shinyanga inashuka daraja.

“Baada ya mazungumzo hayo aliniambia kuwa ngoja kocha wao, Mwinyi Zahera arudi tukamilishe baadhi ya mambo,”aliongeza mchezaji huyo ambaye Simba iliwahi kumfikiria kwenye usajili wa dirisha dogo.

 

Alipoulizwa kuhusina na hilo Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaya alisema kuwa: “Anayehusika na ishu ya usajili ni kocha kwa hiyo yeye ndiye anaweza pia kuwa na jibu sahihi.”

 

Lakini Zahera jana alikuwa bize muda mwingi na hakutoa ushirikiano kwenye hilo ingawa Spoti Xtra linajua kwamba wiki ijayo atamwaga hadharani mbivu na mbichi za usajili wake na wapya wataanza kutua kimyakimya. Habari zinasema kwamba wiki ijayo wachezaji wengi wanaoachwa na Yanga watajua hatma zao ikiwa ni pamoja na kuanza kulipwa chao wanachodai.

 

Kocha huyo aliyeukana uraia wa Congo na kuchukua wa Ufaransa, anataka kumaliza kila kitu mapema kabla ya kwenda Misri kwenye fainali za Afrika mwezi ujao na timu yake ya DR Congo.

 

Tayari Yanga imeshafanya mazungumzo ya awali na wachezaji wanne wa kigeni kutoka Kenya, Rwanda na Zimbabwe ambao wanacheza nafasi za winga, straika, kipa na kiungo na muda wowote kuanzia mwisho wa mwezi huu wanaweza kutua Dar mmoja baada ya mwingine ‘kusinya’.

Comments are closed.