
Katika taarifa iliyojaa hisia aliyoitoa leo Downing Street, Bi May amesema amefanya “kila awezalo” kutekeleza matokeo ya kura ya maoni kuhusu EU ya mnamo 2016. Ni jambo linalosalia kuwa “na majuto mengi” kwamba ameshindwa kutimiza Brexit – Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya, ameongeza — lakini waziri mkuu mpya ndiyo suluhu ” kwa manufaa ya taifa”.

Katika taarifa yake ya kujiuzulu, May amewataka wananchi wenzake kuendeleza muungano uliopo bila kujali tofauti zao za rangi za ngozi.

Sauti yake ilitetereka na alikuwa mwingi wa hisia alipomaliza hotuba yake akisema: “Nitaondoka katika wadhifa huu hivi karibuni lakini imekuwa heshima kubwa maishani mwangu kuhudumu kama waziri mkuu mwanamke wa pili, na bila shaka si wa mwisho.
“Nachukua hatua hii bila ya kuwa na nia mbaya, bali natoa shukurani za dhati na kubwa kutokana na kupata fursa ya kuitumikia nchi ninayoipenda,” amesema May.