
LIGI Kuu Bara imemalizika lakini kuna mechi mbili ngumu za mtoano wa kuwania nafasi ya kucheza michuano hiyo msimu ujao zinapigwa leo Jumapili.
Pamba itacheza na Kagera Jijini Mwanza huku Mwadui ikiwa mgeni wa Geita.

Kocha Mkuu wa Pamba itakayokipiga Nyamagana, Ally Omary Kisaka amesema; “Tumejipanga kwa muda mrefu ili tuweze kupata matokeo dhidi ya Kagera na tutaingia katika mchezo huu tukiwaheshimu sana Kagera kwakua ni timu kongwe katika ligi pia inao wachezaji wazoefu hivyo sisi tutaingia kwa lengo la kupanda ligi,”alisema Kwa upande wake Kocha Msaidizi wa Kagera Sugar, Ally Jangalu alisema: “Mchezo wetu na Pamba tumejiandaa vizuri kuicheza hiyo ‘Playoff’ na tunakwenda kupambana tuone kama tutapata matokeo lakini morali iko juu naamini tutashinda mchezo huo”.
Geita Gold na Mwadui zinamenyana katika Uwanja wa Nyankumbu Boys mkoani Geita. Katibu wa Mwadui Ramadhan Kilao amesema:“ Tunatambua sana umuhimu wa huu mchezo kwamba kama tukifungwa basi tutashuka daraja hivyo hatutakubali kufungwa kirahisi badala yake tutapambana mpaka mwisho.”
Naye Kocha Mkuu wa Geita Gold ,Hassan Banyai alisema; “Wachezaji wangu wako katika hali nzuri na kikubwa nimewaambia wachezaji tuiheshimu Mwadui kisha tucheze mpira naamini tutapata matokeo licha ya kuwa tunacheza na timu ambayo ina wachezaji wengi wazoefu katika ligi lakini hatutajali” alisema. Mechi za marudiano zitapigwa Juni 8