×

Metacha Agomea Benchi Yanga, Amchimba Mkwara Farouk

Metacha Mnata

KIPA mpya wa Taifa Stars na Klabu ya Yanga, Metacha Mnata, ametoa kauli ya kitisho kwa kipa mwenzake raia wa Kenya, Farouk Shikalo kwa kumwambia kuwa anakuja kucheza na siyo kukaa benchi.

 

Kauli hiyo aliitoa ikiwa ni saa chache tangu ajiunge na kambi ya timu hiyo mkoani Morogoro ikijiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na mashindano mengine.

 

Makipa hao wote wamejiunga na Yanga hivi karibuni wote wakisaini mikataba ya miaka miwili wakiungana na kipa Mkongomani, Klaus Kindoki aliyebakisha miezi sita katika mkataba wake.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mnata alisema kuwa kabla ya kusaini Yanga alikuwa anajua anakutana na ushindani wa namba, hivyo amejiandaa vema kuhakikisha anakuwa kipa namba moja mbele ya Shikalo ambaye ni kipa wa timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’.

 

Mnata alisema kuwa anaheshimu uwezo mkubwa alionao Shikalo na wengine aliowakuta katika timu hiyo, lakini amejiandaa vema katika hilo kuhakikisha anafanikisha malengo yake. “Mimi kabla ya kujiunga na Yanga, nilikuwa nafahamu kabisa ninapokuja nitakutana na changamoto kubwa ya ushindani wa namba.

 

“Hivyo, basi nimekuja hapa Yanga kwa ajili ya kucheza katika kikosi cha kwanza na siyo kukaa benchi, licha ya kuheshimu uwezo wa kila kipa aliyepo Yanga. “Nimepanga kuonyesha uwezo wangu kwa kuanzia mchezo wetu wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya AS Vita baada ya hapo ninaamini kocha ataniamini na kunipa nafasi,” alisema Metacha.