
SENETA mwandamizi wa jiji la New York nchini Marekani, Chuck Schumer, amewataka maofisa wa shirika la upelelezi la Marekani (FBI) kufanya uchunguzi kuhusu mtandao wa FaceApp ambao umekuwa ukitumika kubadili picha ya mtu kumuonyesha akiwa mzee au kijana.
Hatua ya Shumer imekuja siku moja baada ya App hiyo kutumiwa na watu maarufu duniani wakiwamo wanamichezo, wasanii na viongozi wa siasa.
Kupitia barua aliyoiweka kwenye mtandao wa Twitter Julai 18, 2019, Schumer alisema kuwa App hiyo inamilikiwa na kampuni ya Urusi ambako ndiko yalipo makao makuu ya kampuni hiyo inayochukua data za maelfu ya picha zinazotokana na utumiaji na kuwapo kwa hatari ya kudukuliwa habari zao.
Ikumbukwe kuwa vyombo vya habari vya Magharibi huhusisha chochote chenye historia ya Urusi kuwa chenye kuhusika na ujasusi.
Kufuatia barua ya Schumer, kampuni ya Wireless Lab ambayo ndiyo wamiliki wa App hiyo, imeshatoa ufafanuzi ikisema ingawa makao makuu ya App hiyo ni Urusi, servers zinazotumika katika kupokea na kutengeneza picha mpya hazipo nchini Urusi.
Kampuni hiyo imenukuliwa na shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) ikisema kuwa wanachofanya ni kukusanya picha maalumu zilizotumwa kwa ajili ya kuzihariri.