
RAIS John Magufuli leo Jumatano, Julai 24, 2019, ameshuhudia makabidhiano ya dhahabu iliyokamatwa nchini Kenya iliyowasilishwa na mjumbe maalum wa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Monica Juma.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika makabidhianayo hayo, Waziri Juma alisema:
“Tunashukuru kwa kumpokea rais wetu kule Chato. Tulipokutana Entebbe mlituamrisha kuwa tusipofanya haraka mtajipangia kukutana, tulipopata simu, nikamuuliza rais nitakuja Chato? Akaniambia ‘huwezi, nitakwenda mwenyewe’ kwa kuwa nyie hamkupanga.
“Leo tuna furaha sana, nilikuwa kwa muda mrefu nikitamani kufika Dar. Tumefika hapa leo kuleta ujumbe kutoka kwa ndugu yako Rais Kenyatta. Amenituma kukuletea wewe ujumbe na pia dada na kaka zetu wa Tanzania kupitia wewe.”

Naye Rais Magufuli baada ya kushudia makabidhiano ya dhahabu amesema:
“Namshukuru Rais Kenyatta kwa upendo na uaminifu mkubwa alionao kwa kurejesha dhahabu yenye uzito wa kilo 35 pamoja na fedha, Rais Uhuru amefanya kitendo cha kiungwana kwa kuturudishia madini yetu ambayo yalikuwa yametoroshwa.
“Navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama vya Kenya kwa kazi kubwa walioifanya.

“Tuliamua kuchukua hatua za makusudi za kuweka mikakati ya kulinda rasilimali zetu za madini ili ziweze kuwanufaisha Watanzania.
“Wa kupongezwa kwa hili ni vyombo vya Kenya, najua wakuu wa vyombo hivyo Tanzania mpo hapa, lazima niwatandike kwa sababu vitu vimetoka Mwanza vimekamatiwa Kenya. Je, vilipobebwa Mwanza na Kilimanjaro vyombo vyetu vilikuwa vinafanya nini?

‘Vitu vya fedha na dhahabu vinahitaji moyo wa jiwe, kiukweli Rais Kenyatta ni muaminifu, kwani vingeweza kupigwa, lakini fedha hizi zimerudi Tanzania baada ya miaka 15. Lakini na mimi mnipongeze, inawezekana wengine wangepiga dili juu kwa juu na wala msingejua.
“Mali za wananchi lazima zirudi kwa wananchi kwa ajili ya maendeleo, Kenya na Tanzania ni kitu kimoja.”
Pia Magufuli alisema Kenya imeahidi kununua unga kutoka Tanzania badala ya mahindi, jambo ambalo alisema ndiyo udugu na urafiki wa kweli.
