
MFALME wa mahojiano Bongo (King Of Interviews), Omary Tambwe maarufu kama Lil Ommy, THE MVP – ametajwa kuwania tuzo kubwa za Star QT Awards 2019, kwenye kipengele cha MTANGAZAJI BORA BARANI AFRIKA MWAKA 2019 huko Afrika Kusini.
Hatua hiyo imekuja baada ya Lil Ommy kuwa mtangazaji mwenye ushawishi mkubwa kwa sasa kupitia kipindi chake cha The Playlist kinachoruka Times Fm 100.5 Dar es Salaam, Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa 10 hadi saa 12 jioni na pia kupitia chaneli yake ya YouTube, LilOmmyTV.
Akizungumzia tuzo hizo zinazotarajia kutolewa Octoba 26 mwaka huu katika ukumbi wa The Edenvale City jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Lil Ommy ‘The MVP’, alisema Star QT Awards zinatolewa kwa mwaka wa sita sasa na amefurahi kuwa miongoni mwa mastaa kutoka Tanzania wanaowania.
“Nimefurahi kuingia kwenye kipengele cha kuwania tuzo ya Mtangazaji Bora Afrika, nashukuru Mungu, mashabiki wanaosikiliza na kutazama mahojiano ninayofanya na mastaa mbalimbali katika chaneli yangu ya YouTube ambapo mpaka sasa nimefikisha watazamaji zaidi ya milioni 30 dunia nzima na wafuasi zaidi ya laki 5 kwenye Instagram,”
“Pia naishukuru familia yangu ya Times FM, Mkurugenzi wangu Mr Rehure Nyaulama aliyeniamini toka mwanzo pamoja na ushirikiano wa wafanyakazi wenzangu na timu yangu ya kipindi bora cha burudani cha The Playlist kama Alen Donald, Ammy Gal, Nick Millz na Dj D Slash, naomba watu wote mnipigie kura kupitia tovuti yao ya www.starqt.com/awards kuanzia Agosti 14 mwaka huu,” anasema Lil Ommy.