×

PADRI AONGOZA MISA YA KUMBUKUMBU MAMA WA SHIGONGO

Padri wa Parokia ya Ilunga, Bagamoyo, Godefroy Masengo, jana akiongoza misa ya kumbukumbu ya kifo cha mama wa Mkurugenzi wa Global Group, Eric Shigongo, Asteria Kapela.

PADRI wa Parokia ya Ilunga, Bagamoyo, Godefroy Masengo, jana Julai 27, 2019 aliongoza misa ya kumbukumbu ya kifo cha mama wa Mkurugenzi wa Global Group, Eric Shigongo, Asteria Kapela iliyofanyika nyumbani kwa mtoto mkubwa wa marehemu, Leah James Bukumbi, Bagamoyo mkoani Pwani.

Picha kubwa ikionyesha mama wa Mkurugenzi wa Global Group, Eric Shigongo, Asteria Kapela.

Mama huyo wa Shigongo aliyezaliwa mwaka 1931, alifariki dunia Julai 27, 2018 hivyo jana ndugu, jamaa na marafiki walikusanyika pamoja kukumbuka na kusherehekea maisha ya aliyoishi mama huyo kabla ya kuitwa na Mwenyezi Mungu.

 

Katika mahubiri yake, Padre Masengo aliwakumbusha ndugu, jamaa na marafiki waliohudhuria ibada hiyo kumkumbuka mama Asteria kwa kuyaenzi yale mema aliyoyatenda hapa duniani.

Padri Godefroy Masengo akifanya maombi wakati wa misa.

Alisema, marehemu Asteria alikuwa ni mtu wa kupenda umoja, aliyependa kuwaunganisha wanaye wote, aliyekuwa mwaminifu na mwenye kumtanguliza Mungu katika kila jambo.

 

“Hii inaonesha ni jinsi gani mama huyu alikuwa ni mwaminifu, alikuwa na umoja, alikuwa na upendo na mwenye kumtegemea Mungu katika kila jambo na ndio maana tunashuhudia haya mambo kupitia watoto wake hawa.

Mhariri wa Gazeti la Amani, Eric Evarist, akisoma neno la Mungu katika misa hiyo.

“Hivyo niwasihi ndugu zangu kuishi kwa mfano wa mama huyu. Tuwe wamoja, kwani hakuna jambo linaweza kufanikiwa kama watu hawakai kwa umoja. Hakuna jambo linaweza kufanikiwa kama watu wataishi bila upendo, uvumilivu na uaminifu,” alisema padre huyo.

 

 

Akizungumza kwa niaba ya familia mara baada ya ibada hiyo, Shigongo alimshukuru Mungu, akamshukuru padre kisha akawashukuru ndugu jamaa na marafiki walioweza kufika katika ibada hiyo ambayo anaamini inamfurahisha mama yao katika makao yake ya milele.

Mkurugenzi wa Global Group, Eric Shigongo (wa pili kutoka kulia) akiwa na Mjasiliamali, Dr. Didas Lunyungu (kulia), Nzungu (wa pili kutoka kulia) na Mhariri wa Gazeti la Amani, Eric Evarist (kushoto)

“Huko alipo naamini mama anafurahia kwamba wanaye bado tunamkumbuka, tunamuomba Mungu azidi kudumisha umoja wetu, tuweze kufanya kumbukumbu hii kila mwaka. Nawashukuru wote mliofika kuungana na sisi, nafahamu tulikuwa na majukumu mengine lakini mkatenga muda huu kwa ajili ya kuungana na sisi, Mwenyezi Mungu awabariki sana,” alisema Shigongo.

Akimzungumzia marehemu mama yake, Shigongo alisema kwake yeye bado anaendelea kumtesa moyoni kwani alikuwa naye karibu kwa takriban miaka 10 hadi umauti ulipomkuta.

Ndugu, marafiki wakiwa katika misa

“Yani bado sijawa sawa lakini namshukuru Mungu naendelea kuimarika. Nakumbuka vile nilivyokuwa kila jioni nakwenda nyumbani kwake kumuona kwa kweli bado sijakaa sawa, nawaomba ndugu zangu tuendelee kumuenzi mama kwa yale mazuri aliyotuachia.

“Mama alikuwa anapenda watu, najua kwa wafanyakazi wenzangu waliopo hapa watakuwa ni mashahidi katika hili. Mama huwezi kwenda kwake halafu usile, alikuwa na mkarimu kupindukia ambao hata mimi mwenyewe wakati mwingine naona kama unaweza kunishinda,” alisema Shigongo.

Wafanyakazi wa Global Group wakiwa katika Misa hiyo.

Naye dada yake Shigongo, Leah aliwashukuru ndugu majirani zake na wafanyakazi wa Global Group waliofika kwenye ibada hiyo sambamba na wanakwaya.

“Jamani mimi nampenda sana Mungu, nawapenda majirani zangu, niwashukuru wote kwa kufika na Mungu azidi kuwabariki,” alisema.

(Habari na Erick Evarist | Picha na Sweetbert Lukonge, GPL)

MAGAZETI JULAI 28: NGUZO TATU ZA MAGUFULI / KIKWETE ATIKISWA CCM!