BALOZI wa Tanzania nchini Sweden, Dkt. Wilbroad Slaa, amekemea tabia ya baadhi ya Watanzania kubeza miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya awamu ya tano huku akibainisha kuwa vitendo vya kutumia mitandao ya kijamii kukosoa utendaji wa serikali unawapa shida mabalozi kuitetea nchi huko walipo, kwa sababu vitendo hivyo vinawakatisha tamaa wahisani wanaotaka kuisaidia Tanzania.Slaa ametoa kauli hiyo wakati akifanya mahojiano na kituo cha televisheni cha Star TV wakati wa ziara ya mabalozi wa Tanzania kutoka nchi mbalimbali duniani walipotembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) eneo la Soga mkoani Pwani.
Ametoa mfano kwamba kutokana na kauli aliyoitoa kiongozi fulani ambaye hakumtaja, imesababisha watalii 100 kutoka Sweden kuahirisha safari ya kuja Tanzania kwa ajili ya kutalii.
Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali wapo katika ziara ya kutembelea na kuijonea utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya awamu ya tano kwa fedha za ndani.