×

Lipa Kwa M-Pesa Yaleta Mapinduzi Makubwa

Msemaji Mkuu wa Jeshi la Uhamiaji, Mrakibu Mwandamizi Al-Hajj Ally Mtanda akitoa maelezo kuhusiana na huduma za idara ya Uhamiaji kwa Mkurugenzi wa M-pesa Vodacom Tanzania PLC, Epimack Mbeteni leo jijini Dar Es Salaam, kwenye gulio la M-Pesa (M-Pesa Expo).

 

Kampuni ya mawasiliano ya simu inayoongoza Tanzania, Vodacom, imezindua huduma ya LIPA KWA SIMU katika gulio la M-pesa lililofanyika Mlimani City jijini Dar, wikiendi iliyopita ambapo wateja na umma kwa jumla sasa watanufaika na mfumo wa huduma za M-pesa unaoruhusu malipo kwenda mitandao na mabenki yote.

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa M-Pesa, Epimack Mbeteni amesema Vodacom Tanzania iliona hitaji la kupanua mfumo wa LIPA kwa M-Pesa kutoka katika mfumo wa M-Pesa na  kuanza kupokea malipo kutoka mitandao na benki zote na kufikia katika kuwezesha malipo ya kidijitali katika mifumo ya rejareja na manunuzi mitandaoni.

 

Amesema Vodacom imezindua huduma ya ‘Lipa Kwa Simu’ kuhamasisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali kama njia kuu ya malipo nchini na kuhama kutoka katika utegemezi mkubwa wa fedha taslimu uliopo sasa.

 

“Lipa kwa Simu ni hatua ya kimapinduzi iliyochukuliwa na Vodacom kuelekea katika kujenga jamii isiyotumia fedha taslimu kwa kusaidia ushirikiano wa malipo katika mitandao na benki zote.  “Kwa kutumia huduma ya Lipa kwa Simu, wafanyabiashara na wamiliki wa biashara wanaweza kupokea malipo kutoka kwenye mitandao na benki zote na kuongeza ufanisi na usalama katika biashara zao.

 

“Kwa upande wa wateja, bila kujali unatumia mtandao gani, sasa unaweza kufanya malipo kupitia mfumo wa LIPA kwa kutumia gharama za kawaida za kuhamisha fedha. Jambo ambalo linaondoa mahitaji ya kutembea na kiasi kikubwa cha fedha taslimu,” amesema Mbeteni.

 

“Vodacom imewezesha LIPA kwa Simu kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara wa sekta zote kama baa, hoteli, migahawa, supermarket, vituo vya mafuta, kumbi za sinema, maduka ya dawa, maduka ya vifaa vya ujenzi na kadhalika.

 

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo ameipongeza huduma hiyo inayotolewa na M-Pesa na kusema kwamba imerahisisha na kuleta ufanisi katika mifumo ya malipo ya umma kwa sababu sasa wateja wanaweza kulipia bili, tozo na huduma nyingi za kijamii kupitia mfumo huu wakiwa sehemu yeyote ile, iwe nyumbani au maeneo yao ya kazi.

 

Gulio la M-Pesa lililofanywa na Vodacom lilivutia maelfu ya wateja, wafanyabishara na jamii kwa jumla ambao walijifunza na kuona jinsi ambavyo mfumo mpya wa Lipa kwa Simu umerahisisha huduma ya malipo nchini.

Na Neema Adrian, Dar.