×

Hudefo Yabaini Changamoto Za Wazee

Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Human Dignity and Environmental Care Foundation (Hudefo), Sara Pima (kulia) akiwa na Asha Said (76) alipomtembelea nyumbani kwake Sinza C jijini Dar es Salaam.

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Human Dignity and Environmental Care Foundation (Hudefo) limebaini changamoto nyingi zinazowakabili wazee.

Shirika hilo linalojihusisha na utu na mazingira lenye makao makuu jijini Dar es Salaam,  limebaini changamoto hizo mwishoni mwa wiki iliyopita katika wiki ambayo huanza kuadhimishwa Oktoba Mosi kila mwaka.

…Akiwa na Bi. Fatuma Mzee (73) alipomtembelea nyumbani kwake Sinza A.

Akizungumza na gazeti la Uwazi, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Sara Pima,  amesema katika kuadhimisha siku hiyo,  waliwatembelea wazee katika maeneo mbalimbali  jijini  Dar es Salaam yakiwemo Sinza, Magomeni, Ubungo na mengineyo.

Katika ziara hiyo Hudefo walizungumza na baadhi ya wazee akiwemo Bi. Fatuma Ally (73) wa Sinza A, Asha Said (76)  naye akiwa mkazi wa Sinza C, ambapo Sara amesema baadhi ya changamoto walizokumbana nazo ni pamoja na wazee hao kukosa bima za afya na wengine kuwa na bima ndogo ambazo zinaishia kwenye kumuona daktari tu na si kupata dawa.

Wazee hawa nao walitembelewa na taasisi hiyo.

Ameongeza kwamba changamoto nyingine ni wazee hao kutengwa katika masuala ya msingi kwenye jamii na kudharauliwa. Pia alisema kwamba changamoto nyingine wanayokutana nayo ni umaskini ambapo wazee wengi nguvu zao zimepungua,  hivyo mara nyingi kipindi hicho hukosa nguvu za kuendelea kutafuta mali na walizonazo zinaanza kupungua na hata kutoweka.

 

Tatizo lingine walilogundua ni wazee wengine kunyanyapaliwa kutokana na mwonekano wao ambao hauvutii tena.

Katika maadhimisho ya siku hiyo mwaka huu,  Hudefo wamekuja na kauli mbiu isemayo “Wazee ni wa thamani, tuwatunze, tuwathamini,  tuwajali na kuwatumia kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi”.

 

HABARI/PICHA NA MWANDISHI WETU.