NI kawaida kukuta maisha wanayoishi Wanasiasa ni tofauti na wapiga kura wao lakini sio hivyo kwa aliyekuwa Rais wa Uruguay, Jose Mujica ambae anaishi kwenye maeneo ya mashambani na anatoa sehemu kubwa ya kipato chake kusaidia watu masikini.
Kutokana na hulka ya Viongozi na watu wengi kutaka kutukuzwa na kupewa kipaumbele hasa katika kupata huduma za kijamii, Mujica alikuwa akikaa kwenye foleni kutaka kumuona daktari katika hospitali ya umma (si daktari wake binafsi).

Analindwa na Polisi wawili na mbwa na aliikataa kukaa kwenye nyumba ya Serikali aliyopewa na badala yake kaenda kuishi kwenye nyumba ya mke wake huko mashambani ambako kuna mazingira ya kimasikini sana ikiwemo barabara mbovu nje kidogo ya mji wa Montevideo.

Mujica anatoa asilimia tisini 90% ya mshahara wake wa kila mwezi kusaidia watu masikini huku akisema ‘naweza kuonekana kama mzee wa jadi lakini maisha haya nimeyachagua mwenyewe, naweza kuishi vizuri na kile nilichonacho.

Matumizi yake hayazidi shilingi milioni moja laki nne za Kitanzania ambapo kwenye kuorodhesha kiwango cha kipato cha kila kiongozi kwa mwaka na mali binafsi ikiwa ni lazima nchini humo kwa viongozi mbalimbali wa serikali mwaka 2010, alikutwa na kiasi cha dollar $ 1,800 tu kiasi ambacho hakizidi shilingi milioni tatu za kitanzania.
Mujica aliwahi kupigwa risasi mara sita na alitumikia kifungo miaka 14 jela ambapo muda wake mwingi kizuizini alikua katika mazingira magumu na kutengwa, mpaka alipoachiliwa huru mwaka 1985 wakati Uruguay ilivyorudi kwenye demokrasia.

Akiwa jela Mujica anasema hali ile ilimbadilishia mtazamo wake juu ya maisha na anakwambia ‘mimi naitwa rais maskini lakini mimi wala sihisi umaskini wowote, watu masikini ni wale ambao kazi yao ni kuishi maisha ya gharama ambayo inawasababisha kufanya kazi sana ili waendelee na maisha ya gahrama na kupata zaidi’ Mujica aliwalaumu viongozi wengi wa dunia ya kuwa na “upofu wa kutaka kukua na matumizi, kiasi kwamba isipokua hivyo itakuwa mwisho wa dunia.