WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema siku za mtu anayejiita ‘Kigogo’ kwenye mitandao ya kijamii ambaye amekuwa akiwazushia mambo mazito viongozi wa Serikali, zinahesabika.
Lugola ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Novemba 2, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Kigogo ni jina linalotumiwa na mtu katika mitandao ya kijamii ya Twitter na Instagram; “Kuna mtu anayejiita Kigogo kwenye mtandao wa Twitter kazi yake kubwa ni kuikosoa Serikali katika mambo mbalimbali, nasema siku zake zinahesabika,” amesema Lugola.
Lugola amesema kama ilivyo kalenda, hata siku za mtu huyo zinahesabika, akibainisha kuwa atakamatwa. Lugola alimzungumzia Kigogo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu makosa ya mtandao.
“Kuna baadhi ya Watanzania bado wana mtindo unafika wakati wa uchaguzi wanapotosha jamii na kutoa kauli za kuvunja amani kwa kisingizio cha kampeni au uchaguzi, safari hii hiyo nafasi hakuna, wakorofi kabisa tutawatumbukiza kabisa kwenye hayo maji yanayowasha,tutawaogesha,” amesema Lugola.