Leo Novemba 3, 2019 Rais Dkt. John Magufuli amefanya uteuzi wa viongozi katika nafasi mbalimbali ambapo amemteua Charles Kichele kuwa Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) akichukua nafasi ya Prof.Mussa J.Assad ambaye uteuzi wake wa miaka mitano unaisha Novemba 4 mwaka huu.
Uteuzi huo umetangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi John Kijazi, Ikulu jijini Dar es salaam ambapo kabla ya uteuzi huo Kichele alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, huku nafasi yake hiyo ikichukuliwa na Katalina Tengia Levekati ambaye alikuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
Aidha Magufuli amemteua Kamishina wa kazi Kanari Francis Leonard Mbindi kuwa Kamishina wa Kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Gabriel Warata ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na majaji 12 wa Mahakama Kuu. Hafla ya kuapishwa kwa viongozi waliochaguliwa inatarajiwa kufanyika siku ya Jumatatu Novemba 4 mwaka 2019. #GLOBALHABARI