Tamasha Kubwa La Vijana Dar… Siku Zinahesabika
HOMA ya lile tamasha kubwa la wanachuo na vijana kutoka pande mbalimbali imezidi kupanda kwani sasa zinahesabika siku tu ili lifanyike Novemba 15, mwaka huu kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar.
Tamasha hilo kubwa la kiroho linaloendana na burudani ya muziki linaandaliwa na Kanisa la TAG–Victory Christian Centre Tabernacle kwa kushirikiana na Jumuiya za Kikristo na Serikali za wanafunzi wa vyuo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Mchungaji Dkt. Huruma Nkone amesema tamasha hilo ambalo limekuwa likitumika kuwapa moyo na kuwajenga kiroho vijana hao, limeshafanyika mara nane kwa mafanikio makubwa.
Dkt. Nkone ambaye atakuwa mhamasishaji wa kuwajenga kiroho na kiakili vijana hao, amewataja wazungumzaji wengine kuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Global Group, Eric Shigongo, Samuel Sasali, Dk. Hellen Gwambaye na Salome Msimbe.
Aliongeza kuwa amehakikishiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda uwepo wa usalama wa kutosha kwa watakaohudhuria tamasha hilo wao pamoja na mali zao.
Tamasha hilo pamoja na kuwajenga kiuzalendo vijana hao, litapambwa na burudani kutoka makundi mbalimbali ikiwemo Zabron Singers, Upendo Nkone, Joel Lwaga, Walter Chilambo, Students Mass Choir, Beda Smith, Hype Squad Dancers, Rivers of Joy International na Mkhululi Bhebbe kutoka sauzi Afrika.
Kwa upande wake Shigongo, alisema tamasha hilo lina msingi mkubwa sana wa kuwajenga kiroho vijana hao na kusema usipowajenga vyema vijana si rahisi kupata taifa bora.
“Vijana wanatakiwa kupewa hamasa na kujengwa kiroho ili waweze kufikia malengo yao. Tukiwa na taifa lenye watu wenye hofu ya Mungu, ni lazima tupige hatua kubwa ya kimaendeleo.
“Tatizo kubwa lililopo hapa nchini kwa sasa ni vitu kama kukosa uaminifu, hivyo kutoaminiwa jambo ambalo linawafelisha wengine kwenye koneksheni za mafanikio,” alisema Shigongo na kuwataka vijana kufika kwa wingi kwenye tamasha hilo ambalo kiingilio ni bure.
TAZAMA SHOO YA MKHULULI BHEBHE
Comments are closed.