
DROO kubwa ya Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili inatarajiwa kuchezeshwa Septemba 27 mwaka huu, hiyo ikiwa na maana kuwa siku 13 tu kuanzia sasa, mjengo huo wenye thamani ya mamilioni ya shilingi utampata mwenyewe.
Nyumba hiyo ya kisasa imejengwa katika eneo la Bunju B nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Meneja Mkuu wa Global Publishers, ambao ndiyo waendeshaji wa zoezi hilo kubwa kabisa nchini, Abdallah Mrisho, alisema jana kuwa maandalizi yote kwa ajili ya hafla hiyo ya aina yake yamekamilika na kinachosubiriwa ni siku yenyewe ya tukio, ambayo itakuwa ni Jumatano.

“Tumekamilisha kila kitu, kilichobakia sasa ni kuwaomba wasomaji wa magazeti yetu ya Ijumaa Wikienda, Amani, Uwazi, Risasi, Championi na Ijumaa kukata kuponi zao za mwishomwisho na kuzituma kwetu haraka iwezekanavyo. Kwa wale wa mikoani, kuponi zao wazipeleke kwa wakala wetu ambao wako kila sehemu nchini.
“Kwa wale wa Dar wazilete kuponi zao katika ofisi zetu zilizopo Bamaga, Mwenge na wazikabidhi kwa watu maalum wanaozipokea. Huu ni wakati wa kuhakikisha hawakosi nakala zao kwa vile muda umeshaisha. Wiki mbili zilizobaki wahakikishe hakuna mtu anayeziacha kuponi zake bila kuzileta kwetu, kwa sababu huenda ile utakayoiacha nyumbani, ndiyo iliyokuwa ya mshindi,” alisema Mrisho.
Nyumba hiyo ya kisasa imejengwa Bunju B, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam ikiwa na thamani ya mamilioni ya shilingi na itakuwa ni ya pili kutolewa na Global Publishers, kwani katika bahati nasibu ya kwanza iliyofanyika mwaka jana, mjengo kama huo ulitolewa.
Shinda Nyumba Droo ya Kwanza Yafanyika, Washindi Wapatikana
Aliyeshinda katika bahati nasibu hiyo ya kwanza alikuwa ni mwanamama mjasiriamali, Nelly Mwangosi mwenyeji wa Iringa ambaye mjengo wake ulijengwa eneo la Salasala, pia nje ya jiji.
Washindi wa Shinda Nyumba wakabidhiwa Zawadi zao
Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili inafanyika baada ya kuwepo kwa droo ndogo tano zilizochezeshwa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam ambako zaidi ya wasomaji 30 wa magazeti ya Championi, Ijumaa, Risasi, Uwazi, Amani na Ijumaa Wikienda waliibuka na zawadi za aina mbalimbali zikiwemo pikipiki, televisheni kubwa, simu za kisasa za mikononi, dinner set na ving’amuzi.