×

Baba Azimia Baada ya Mwanaye Amebakwa – Video

INAUMA sana! Baba mmoja aliyejulikana kwa jina la Rashidi mkazi wa Manzese, Dar amejikuta akipoteza fahamu kutokana na tukio la ubakaji wa mwanaye, Ijumaa Wikienda linakupa habari kamili.

Akizungumza na Ijumaa Wikienda, mama mzazi wa mtoto huyo, Sofia alisema siku ya tukio yeye alikuwa kwenye biashara zake ndipo alipopigiwa simu na mume wake na kuelezwa kilichotokea.

“Nafanya biashara ndogondogo, nilipotoka siku hiyo nilimuacha mwanangu na baba yake wakiwa salama, ilipofika saa tatu asubuhi mume wangu alinipigia simu kunieleza kuwa kuna tukio nyumbani la mwanangu kubakwa.

“Kiukweli tukio hili lilifunga mtaa kwani baada ya kurudi nyumbani nilikuta watu wamejaa huku wakiwa wamemzunguka mtuhumiwa pamoja na mtoto wangu,” alisema mama huyo.

Aliendelea kueleza kuwa kutokana na mshtuko na kukasirishwa na kitendo hicho, mumewe alipoteza fahamu hivyo kumkuta naye amezingirwa na watu wakimpepea ili aweze kuzinduka.

“Mume wangu alipozinduka akaniambia kuwa alimtuma mtoto wetu huyo dukani kununua sukari. Lakini alitumia muda mrefu, ikabidi atoke kumtafuta ndipo alipomkuta akitokea kwenye chumba cha huyo Tola, ambaye chumba chake kipo jirani na chetu, akaamua kumuita mzee mmoja jirani na kumwambia amuulize Tola mtoto wangu alikuwa akifanya nini chumbani kwake?

“Tola alipoulizwa akawa anamuomba mume wangu amsamehe huku akiwa amepiga magoti, alipoulizwa asamehewe kwa kosa gani? Hakujibu kitu, ndipo wakamkagua mtoto na kukuta kuwa amebakwa.

“Ikabidi twende Hospitali ya Tandale, mtoto akapimwa na kugundulika kuwa ameingiliwa zaidi ya mara tatu. Mtoto alipoulizwa akasema Tola ndiye huwa anamfanyia mchezo huo na kumkataza asiseme kwa mtu yeyote na akisema atamuua.

“Ikabidi tukaripoti polisi na mtuhumiwa akakamatwa, lakini nashangaa mpaka sasa mtuhumiwa bado yupo pale na mwanangu bado anaugulia. Naiomba Serikali iliangalie hili suala kwa sababu mpaka leo baba yake hali yake ni mbaya kutokana na lile tukio.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa Wa Mvuleni, Dar Neema Iddy alikiri kupata taarifa za mtoto huyo kuwa amebakwa.

“Nilipata taarifa kutoka kwa mama wa mtoto, aliniambia kuna tatizo nyumbani kwake. Nikaenda pale na kumkuta mtuhumiwa akiwa amezungukwa na watu, nilipomuona nikamkumbuka kwamba ameshawahi kufanya tukio kama hili mara ya tatu.

“Tukio lingine alimfanyia mtoto wa kiume, alikamatwa akapelekwa hapohapo kituo cha Polisi Urafiki, akatolewa, tulipouliza tukaambiwa kesi bado inaendelea. Naiomba Serikali imchukulie hatua huyu jamaa” alisema.

 

STORI: NEEMA ADRIAN, DAR