The House of Favourite Newspapers

SBL YAHIMIZA USALAMA BARABARANI

KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL), imetoa vifaa vya usalama barabarani na elimu kwa madereva wa mabasi na waendesha bodaboda mjini Moshi, ikiwa ni mchango wa kampuni hiyo katika kupambana na ajali za barabarani.

 

Hatua hiyo ni mwendelezo wa kampeni ya nchi nzima ya kampuni ya SBL kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara na hususan madereva inayojulikana kama ‘Usitumie Kilevi na Kuendesha Chombo cha Moto’.

 

Utoaji huo wa vifaa ulifanywa na Mkurugenzi wa Mahusiano kwa Umma wa kampuni hiyo, John Wanyancha na kushuhudiwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kilimanjaro, Zauda Mohamed.

 

Vifaa vilivyotolewa ni makoti ya usalama, stika, vipeperushi vyenye ujumbe juu ya usalama barabarani na program za elimu zilizotolewa kupitia redio na kwenye vyuo vya elimu ya juu mjini Moshi.

“Tunapoelekea msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, SBL inapenda kuwakumbusha wateja wake na umma kwa ujumla kusherehekea sikukuu zinazokuja kistarabu kwa kuhakikisha hawaendeshi vyombo vya moto baada ya kutumia kilevi,” alisema Wanyancha.

 

Kwa upande wake, Kamanda wa Usalama Barabarani Mkoa wa  Kilimanjaro aliishukuru SBL kwa kuandaa kampeni hiyo na kuongeza kuwa kwa kulishirikisha jeshi la Polisi kampuni hiyo inaiunga mkono Serikali katika kutoa elimu ya usalama barabarani na pia kupambana na ajali zinazosababishwa na unywaji usio wa kistarabu.

 

Kamanda Zauda aliwaonya madereva na watumiaji wengine wa barabara wanaotumia kilevi na kuendesha vyombo vya moto bila kufikiria athari za kufanya hivyo na kusisitiza kuwa jeshi la Polisi halitawavumilia watu wa aina hiyo hasa katika kipindi hiki tunapoelekea msimu wa sikukuu.

 

“Hatupendi kuona uharibifu wa mali, majeruhi au mtu kupoteza maisha kwa sababu ya ajali zinazosababishwa na utumiaji wa pombe usio wa kistarabu na sababu nyinginezo,” alisema Zauda.

Na Neema Adrian.

Comments are closed.