
BAADA ya penzi lao kuvunjika na kila mmoja kuwa na uhusiano na mtu mwingine, msanii wa muziki wa RnB, Juma Mussa ‘Jux’ amegoma kufuta picha za zilipendwa wake, Vanessa Mdee ‘Vee Money’ kwenye akaunti yake ya Instagram akisema anakumbuka vitu vingi vya furaha.

Akizungumza na Amani, Jux alisema mara nyingi watu wanapoachana, basi wanahakikisha wanafuta picha zote za wapenzi wao kwenye simu zao na akaunti zao, lakini kwa upande wake hilo haliwezekani kwa sababu picha hizo zinamfanya akumbuke mambo mengi mazuri waliyokuwa wakiyafanya enzi za penzi lao.

“Siwezi kufuta picha za Vanessa kwenye akaunti yangu, kwa sababu kuna nyakati f’lani za nyuma bado nazikumbuka, isitoshe zile picha nilikuwa naziposti kwa mapenzi yangu, yaani kipindi hicho ninaziposti nilikuwa kwenye furaha na Vanessa, sasa kwa nini leo nizifute? Haitakuja kutokea,” alisema.
Stori: Imelda Mtema