
TONI-ANN SINGH ameshinda Taji la 69 la Shindano la Malkia wa Urembo la Miss World. Ni mara ya kwanza katika historia kwamba mwanamke mweusi anamiliki mataji ya Miss USA, Miss Teen USA, Miss America, Miss Universe na Miss World.
Shindano la Miss World 2019 limefanyika juzi Desemba 14, 2019, katika Ukumbi wa ExCeL London jijini London, Uingereza, ambapo mrembo huyo wa Jamaica alitwaa taji.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 23 ni mzaliwa wa eneo la St Thomas nchini Jamaica, ni mhitimu Chuo Kikuu cha Florida alipokuwa akisoma masomo ya saikolojia na anapanga kusomea utabibu na kuwa daktari.
Hii ni mara ya nne kwa Jamaica kupata taji hili na mara ya mwisho ilikuwa mwaka 1993. Kabla ya hapo ilichukua taji hilo mwaka 1963 na 1976.

Toni-Ann aliwafurahisha majaji katika hafla hiyo mjini London baada ya kuimba wimbo wa Whitney Houston wa ‘I Have Nothing’, na kujibu maswali mbalimbali.
Alisema: ”Hii ni kama ndoto, nimeshukuru sana. Chochote kile munachokiona ndani yangu, ahsanteni, niko tayari kuanza kazi”.
Aliwashinda wagombea wengine 111 wa taji hilo waliokuwa wakiwakilisha mataifa yao, na kuwa mshindi wa nne wa Jamaica tangu shindano hilo lizinduliwe.
Alipoulizwa na jaji Piers Morgan iwapo angependelea kuwa mwimbaji, alisema: “Iwapo milango itafunguliwa nitaingia.”
Waliochukua nafasi ya pili na ya tatu walikuwa ni Ophely Mezino kutoka Ufaransa na Suman Rao kutoka India.
Kitu kimoja kilichovutia hisia za watu mitandaoni ni jinsi malkia wa urembo wa Nigeria alivyotoa hisia zake kufuatia ushindi wa Toni-Ann.
Nyekachi Douglas, ambaye alishika nafasi ya tano alirukaruka na kupiga kelele za furaha wakati mshindi alipotangazwa.
Tanzania iliwakilishwa na Sylivia Sebastian.