
DUNIANI kila mtu ana staili yake, ukihojihoji sana unaweza usipate majibu na ukaitwa mbea! Mtoto mzuri kunako Bongo Fleva, Irene Louis ‘Lyyn’ ameonesha jeuri ya fedha ambayo kimsingi ukimweka kwenye mizani, utajiri wake haufanani na sanaa yake, IJUMAA WIKIENDA linashuka na habari kamili.
UBUYU WA AWALI
Awali, IJUMAA WIKIENDA lilitonywa kuwa, Lyyn ameondoka katika mjengo aliokuwa akiishi Mbezi-Goba jijini Dar na amehamia kwenye mjengo wa kifahari zaidi huko Mbezi-Beach jijini Dar.
Kama hiyo haitoshi, mtoa taarifa alizidi kwenda mbele kwa kueleza kuwa, nyumba hiyo amepangishiwa na kigogo mmoja na hataki kabisa kujulikana kwa watu.

“Lyyn siyo mwenzetu jamani, anaishi kama bilionea vile. Sasa hivi amehama kule Goba alipokuwa akiishi, amepangishiwa bonge la mjengo huko Mbezi- Beach! Yaani huyo mwanaume wake ana pesa balaa na hataki kabisa kujulikana kwa watu, anafanya mambo yake kimyakimya,” alisema mtu wa karibu wa Lyyn.
IJUMAA WIKIENDA LATINGA…
Gazeti la Ijumaa Wikienda lilifanikiwa kufika mpaka Mbezi-Beach anakoishi bishosti huyo na kushuhudia kweli mrembo huyo anaishi vizuri.
Picha linaanza, Ijumaa Wikienda lilishuhudia mjengo wa kifahari anaoishi mrembo huyo ukiwa na bwawa matata la kuogelea (swimming pool).
Mbali na mjengo huo kuwa kwenye eneo la mijengo ya kifahari ushuani, Ijumaa Wikienda lilishuhudia una nafasi ya kutosha na katika parking kukiwa kumependeza kwa kupambwa na magari manne ya kifahari ya mrembo huyo.
Ukiachana na yale ya zamani, Ijumaa Wikienda lilishuhudia ndinga lake jipya aina ya Touareg V6.

Baada ya kupata picha kadhaa za mjengo huo wa kifahari na mandhari yake ya kistaa, Ijumaa Wikienda lilipata nafasi ya kuzungumza na mlinzi wa mjengo huo ambaye hakupenda kujitambulisha kwa majina.
Ijumaa Wikienda: Kaka habari? Official Lyyn tumemkuta?
Mlinzi: Ndiyo yupo, tena ameingia sasa hivi ndani.
Ijumaa Wikienda: Naomba utuitie, mwambie waandishi wa habari kutoka Global wanahitaji kuzungumza naye.
Mlinzi: Sawa (anaenda).
BAADA YA DAKIKA 10 ANARUDI…
Mlinzi: Amesema mje siku nyingine, kwa sasa hawezi kuzungumza chochote, amechoka.
Ijumaa Wikienda: Sawa, ila mwambie atoke tu mara moja, hatutatumia muda wake mwingi.
Mlinzi: Hapana, dada hawezi kutoka, halafu si mnaona jinsi alivyopaki hili gari lake? Yaani hapa anatoka tena sasa hivi, kwa hiyo naomba tu mje siku nyingine kama alivyosema mwenyewe.
Ijumaa Wikienda: Haina shida, sasa hii nyumba mbona kubwa hivi anaishi na nani?
Mlinzi: Anaishi yeye na ndugu zake.
Ijumaa: Ooh! Kweli, ndiyo maana naona wasichana na watoto mbalimbali wanatoka humo ndani. Basi sawa tutarudi kipindi kingine.
Mlinzi: Karibuni sana.
MASWALI YA IJUMAA WIKIENDA
Baada ya Ijumaa Wikienda kushuhudia mjengo huo, lilipata maswali mengi kumhusu mrembo huyo ambayo yanahitaji majibu ya kina.
Swali la kwanza; Ni nani anayempa jeuri hiyo? Na je, yupo tayari kumpa jeuri hii katika hatua ya urafiki tu kabla ya ndoa?
Swali la pili; Kwa nini aliamua kuhama Mbezi-Goba?
Swali la tatu; Kwa nini mwanaume huyo anayempa jeuri hataki kuonekana?
Swali la nne; Lyyn ana nyimbo 4 tu alizofanya video na 2 ni audio, zinaweza kumpa shoo ya kumuingizia kipato cha kuishi maisha ya kitajiri kiasi hicho?
Maswali hayo yote yanafikirisha, lakini hata hivyo, hivi karibuni mrembo huyo alitembelea Global Publishers na alipangua baadhi ya maswali, hebu tumsikie;
Ijumaa Wikienda: Nasikia umehama kule Mbezi-Goba, ni kweli?
Lyyn: Yah! Ni kweli.
Ijumaa Wikienda: Umehamia wapi?
Lyyn: Nimehamia Mbezi-Beach ila sikuambii ni Mbezi-Beach sehemu gani.
Ijumaa Wikienda: Ni kweli watu wasemavyo kwamba hata huko Mbezi- Beach kakupangishia Mondi?
Lyyn: Hapana jamani, mimi nina mpenzi wangu ambaye ni mfanyabiashara na hapendi kuonekana sana kwa watu. Ndiye anayenigharamikia kila kitu, kama unakumbuka mwaka jana kwenye ‘birthday’ yangu ndiye aliyenizawadia ile gari yangu ya BMW na mwaka huu kanizawadia nyumba ipo Kigamboni (Dar).

Ijumaa Wikienda: Hongera sana! Kwa hiyo, hiyo nyumba ya Goba nani anaishi?
Lyyn: Nimeweka tu watu wa kuiangalia na kufanya usafi kila siku.
TUJIKUMBUSHE
Mrembo huyo ambaye aliwahi kudaiwa kutoka kimapenzi na Mondi, amechipukia kwenye Bongo Fleva mapema mwaka huu akitokea kwenye ‘u-video queen’ aliokuwa akiufanya kabla.
Nyimbo zake anazotamba nazo ni Kama Yote, Chafu, Pepea na Chomeka ambazo ni video huku akiwa na nyingine mbili za audio; Hola Hola na Mapepe.
STORI: MEMORISE RICHARD NA IRENE MARANGO, DAR