
BAADA ya kusaini mkataba wa miaka miwili wa kukipiga Jangwani, mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Ditram Nchimbi amesema atautumia mchezo dhidi ya Simba kuthibitisha kiwango chake.
Mshambuliaji huyo juzi Alhamisi alisaini mkataba rasmi wa kuichezea timu hiyo kwa dau la Sh Mil. 40 kati ya hizo yeye ameambulia Sh Mil 20 pekee huku nyingine zikienda kwa Azam FC iliyokuwa inammiliki kama fidia ya kuvunja mkataba wa miezi aliyoibakiza.
Timu hiyo hadi sasa tayari imefanikisha usajili wa wachezaji ambao ni Tariq Seif, Adeyum Salehe, Niyonzima na Nchimbi mwenyewe baada ya mapendekezo ya benchi la ufundi la timu hiyo kutolewa huku wadhamini wao GSM wakifanikisha usajili huo.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Nchimbi alisema kuwa muda mrefu alikuwa na ndoto za kuzichezea klabu kubwa za Simba na Yanga ambazo zimetimia kwa yeye kutua kukipiga Jangwani katika dirisha dogo lililofunguliwa Jumatatuiliyopita.
Nchimbi alisema kuwa amejiunga Yanga kwa ajili kuipa mafanikio na kati ya hayo ni kuhakikisha anaipambaniam timu hiyo iweze kutwaa taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara, pia kuwafunga Simba mara watakapokutana nao ambayo ndiyo kiu ya Wanayanga wote.
“Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutimiza ndoto zangu nilizoziweka za kuichezea mojanya klabu kubwa hapa nchini ambazo ni Simba na Yanga, hivyo ninafuraha kubwa kujiunga na Yanga katika usajili huu wa dirisha dogo.
“Lipo wazi kabisa hakuna mchezaji asiyetamani kuzichezea hizi klabu kubwa mbili hapa nchini, kila mchezaji anajituma na kupambana ili azichezee timu hizo kama ilivyokuwa kwangu, nina furaha kubwa kujiunga na Yanga.
“Huu ni muda muafaka kwangu kuwathibitishia wale wanaobeza kiwango changu na nitawathibitishia mara nitakapoanza kuichezea timu yangu mpya ya Yanga na mara tutakapokutana na wapinzani wetu Simba.
“Nimejiunga na Yanga nikijua kabisa nakwenda kwenye timu yenye ushindani wa namba, hivyo nimejipanga na kikubwa ninataka kuonyesha ushindani,” alisema Nchimbi.
Stori na Wilbert Molandi, Dar es Salaam