×

Hawa Wamekula 6, Bado Nyie

 

BOSI mpya wa Simba, Mbelgiji Sven Vanderbroeck jana alianza majukumu yake ndani ya klabu hiyo kwa mkwara mzito baada ya kuwachapa Arusha FC mabao 6-0.

 

Simba imeanza kupasha misuli ikiwawinda Yanga wanaotarajia kukutana nao Januari 4, na jana baada ya mchezo baadhi ya mashabiki walisikika wamesema: “Hawa wamekula 6, bado nyie Yanga.”

 

Simba walipata ushindi huo mzito kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho (FA) katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar.

Huu ni ushindi wa kwanza unapata benchi la ufundi jipya la Simba tangu wakabidhiwe kuliongoza jahazi la timu hiyo.

 

Kwenye mechi hiyo ambapo Simba iliwakosa baadhi ya mastaa wake, mabao yao yalifungwa na Clatous Chama aliyefunga bao la kwanza akiunga mpira uliotemwa na kipa wa AFC baada ya kutema shuti la Kagere.

 

Mbrazil Gerson Fraga alifunga bao la pili kwa shuti kali akiwa ndani ya 18 kabla ya Deo Kanda kuongoza bao la tatu kwa kumchambua kipa.

Bao la nne lilifungwa na Ibrahim Ajibu aliyepokea pasi ya Chama huku straika Meddie Kagere akifunga la tano na bao la sita likafungwa na Francis Kahata.

 

Mabao yote yalikuwa ya kiwango bora kabisa huku Simba wakitawala mchezo huo. Sasa Wekundu hao wametinga hatua ya 32 bora ya michuano hiyo.

 

Kikosi cha Simba kilichoanza: Beno Kakolanya, Haruna Shamte, Shomary Kapombe/Kennedy Juma, Pascal Wawa, Tairone Santos, Deo Kanda, Gerson Fraga, Clatous Chama/Sharaf Shiboub, Meddie Kagere/ Wilker Da Silva, Ibrahim Ajibu na Francis Kahata.

 

Arusha FC: Athuman Nyamaka, Said Shilingi, Shaban Mtangi, Salum Mtambo, Rodney Chitopela, James Shangala, John Mbilinyi, Jonathan Masimba, Ajib Mohamed, Mathayo Wilson na Gaspa Mwaipasi.

Leave a Comment