
STAA wa Barcelona, Luis Suarez amewakusanya mastaa wenzake kibao Boxing Day kudhuhuria sherehe ya miaka 10 ya ndoa yake na mrembo, Sofia Balbi iliyofanyika kwenye hoteli ya nyota tano huko kwao Uruguay.
Straika Suarez, 32, na asali wake wa moyo tangu enzi wa utotoni, Sofia 30, walisherehea miaka 10 ya ndoa yao na kuwaalika watu kibao maarufu wakiwamo wachezaji wa Barcelona, Lionel Messi, Sergio Busquets na Jordi Alba.
Kwenye tukio hilo, Luis na Sofia walitengeneza pete maarufu za almasi, ambapo ile aliyokuwa amevaa mume ilikuwa na kifupi cha jina la mkewe, ‘SB’ na ile aliyovaa mke ilikuwa na kifupi cha jina la mume, ‘LS’. Tukio hilo lilihudhuriwa na mchungaji Juan Andres Verde, ambaye ameripotiwa kuwa ni rafiki mkubwa wa familia hiyo.
Kwenye tukio hilo la kumbukumbu ya ndoa yao ambayo walifunga 2009, Suarez na mkewe walipigilia viwalo vya maana kama vile ndio kwanza walikuwa wakioana. Baada ya tukio, Suarez aliwaambia waandishi wa habari: “Hii ni siku muhimu kwetu, kisha akatania. Mke wangu ni beki mgumu sana, siwezi kabisa kumpiga chenga.”
Messi alihudhuria na mkewe mrembo Antonella Roccuzzo na mtoto wao mkubwa, Thiago, saba.
Sergio Busquets alienda na kimwana wake mrembo Elena Galera sawa na ilivyo kwa Jordi Alba aliyekuwa na mrembo wake Romarey Ventura.
Suarez na mkewe Sofia wamefanikiwa kupata watoto watatu, Delfina, (9), Benjamin (6), na Laurato, mwenye miezi 14.