
MWILI wa marehemu Verdiana Mujwahuzi, mama mzazi wa Erick Kabendera, utawasili Bukoba leo tayari kwa maziko yatakayofanyika kijiji cha Kashenge.
Mtoto wa marehemu, Claudius Kabendera, akiongea na mwandishi wa mtandao huu alisema mwili wa marehemu uliosafirishwa kutoka Dar es salaam, Januari 4, mwaka huu, utahifadhiwa katika Hospital ya Mkoa wa Kagera mjini Bukoba.
Ameongeza kwamba siku ya Jumapili mwili wa marehemu utapelekwa Rwamishenyi kwenye nyumba yake aliyokuwa anaishi wakati wa uhai wake ambako itafanyika ibada fupi na mwili huo utalala katika nyumba hiyo hadi siku ya Jumatatu.

Mwili huo utapelekwa katika kijiji cha Kashenge, Kata ya Katoma, aneo ambalo ndipo mume wake alikuwa anaishi kipindi cha uhai wake, na ndipo alizikwa na hivyo yeye atahifadhiwa katika nyumba yake ya milele kwenye eneo hilo.
Wakati huohuo, maandalizi sehemu hiyo yanaendelea ambapo wananchi walikuwa wakiendelea kuchimba kaburi huku vifaa mbalimbali kama matofali, mchanga na maji vikiwa tayari vimewekwa kwa ajili ya ujenzi wa kaburi hilo.
Hata hivyo, mtoto huyo wa marehemu ameonyesha wasiwasi wake iwapo kaka yake, Erick Kabendera, aliyeko mahabusu Dar es Salaam, ataweza kuruhusiwa kumzika mama yake au la.