×

Baba: Yondani ni Mtu wa Kazi, Simba Wazuri Ilaa….

 

SAA tu kwa sasa kabla ya vita iliyokuwa mrefu kukamilika kwenye Uwanja wa Taifa ambapo wilaya ya Temeke itapokea maelfu ya mashabiki. Simba atakuwa mwenyeji wa mchezo huo akimkaribisha Yanga.

 

Kuna mchezaji mmoja tegemeo ndani ya Yanga, Kelvin Yondani huyu ni Mkongwe za Simba na Yanga kwa nyakati tofauti na amepata bahati ya kucheza timu zote mbili ila kwa sasa yupo Yanga.

 

Championi Jumamosi imefanya mahojiano na baba wa kelvin Yondani, mzee Patrick Yondani kuhusu mechi hiyo, huyu hapa anafunguka;

 

MWANAO YUPO YANGA UNAUONAJE UWEZO WAKE?

“Najua mwanangu sio mtu wa maneno ni mtu wa kazi, uwezo wake huwa unaonekana kwa vitendo. Ninamuamini kwa kuwa anajua ataendelea kuwa bora.

 

NAFASI YAKE NDANI YA YANGA KWENYE MECHI YA SIMBA UNAIZUNGUMZIAJE?

“Mwanangu kwa sasa sio mtoto mdogo kwamba hajitambui anapaswa kuongozwa, hapana! Uzoefu unambeba na amecheza mechi nyingi zinazohusu Simba kwa zaidi ya miaka 10, atabebwa na uzoefu na uwezo wake.

 

“Hawa ni wakongwe na wanabebwa na majina yao hivyo wanapokutana hata ikiwa ni mechi ya kirafi ki ni lazima tambo zitawale na kila mmoja avutie kwake hiyo ni asili yao tangu enzi.

 

UMEMWAMBIA NINI KUHUSU SIMBA?

“Anajua majukumu yake lazima ayatekeleze tena kwa umakini wa hali juu ili aendelee kuwa bora na kuifanya timu yake ifi kie malengo iliyojiwekea.

 

“Najua amecheza mechi ngumu na amekuwa akipata nafasi hata kwenye timu ya taifa, haya yote yanatokana na ubora wake akiwa uwanjani na anazidi kuimarika.

 

UNADHANI ATAWEZA KUWA BORA MBELE YA SIMBA?

“Yondani hata umuamshe usiku wa manane mwambie kuna mechi dhidi ya Simba anaimudu bila mashaka. Katika hilo sina mashaka wala hofu.

 

UNAIONAJE MECHI KIUJUMLA?

“Sio mechi nyepesi hata kidogo kutokana na asili ya hawa wawili wanapo-kutana kila mmoja ana lake moyoni. Ila wakitulia na wakacheza soka la darasani itakuwa ya kuvutia ukizingatia kwamba mashabiki watakuwa uwanjani. Ile butuabutua haitoi burudani.

 

KETE YAKO YA USHINDI IPO WAPI?

“Simba wana asilimia 50 sawa na Yanga nitakachofanya ni kuwa katikati bila kumtambua mshindi mpaka pale dakika tisini zitakapokamilika tutamjua.

 

VIKOSI VYAO UNAVIONAJE?

“Vyote vipo vizuri ndio maana wanapata matokeo. Kila timu ina aina ya wachezaji makini na wazuri.

“Simba wao  wana mchezaji Meddie Kagere na Manula (Aishi) wote wapo vizuri kiushindani.

Yanga wao mwanzo waliyumba kidogo ila uwepo wa Haruna Niyonzima, yeye anajua falsafa ya Yanga na nini inataka pia Tariq Seif naye ameanza vizuri ni suala la kusubiri nini kitatokea.

 

KUHUSU FIGISUFIGISU JE, HILI LIPOJE?

“Ngumu sana kutokea kwa mwanangu na ikitokea mtu amenifuata huyo baya litamkuta nadhani atakuwa anataka anipeleke polisi kisa mwanagu.

 

UTAMFANYA NINI?

“Hebu fi kiria mtu anakwambia umwambie mwanao acheze chini ya kiwango itakuwa sawa? Nitampiga na hilo litanifanya nipelekwe polisi, sina hofu nachotaka kuona mwanagu anafanya kazi sawasawa.

 

UNAWAAMBIA NINI MASHABIKI?

“Wajitokeze kwa wingi ila wasiende na matokeo mkononi maana naona wengi wanaipa nafasi Simba kushinda. Ni kweli Simba ipo vizuri ila sio kwenye mechi dhidi ya Yanga ukaipa asilimia 100 ni ngumu kuamini katika hilo dakika tisini ndizo zitaamua.

 

“Watulie kuona burudani, waamuzi nao wafanye haki ili kila mmoja afurahi kufi ka uwanjani na watakaokuwa nyumbani nao wapate burudani,” anamalizia baba Yondani.  

Lunyamadzo Mlyuka, Dar es Salaam

Leave a Comment