×

Kariakoo Derby: Hawa Watu ni wa Kuchunga Sana!

KUELEKEA katika mchezo wa leo pale Uwanja wa Taifa kati ya Simba na Yanga, kuna baadhi ya nyota wa kigeni tu ambao kila timu inapaswa kuwaangalia kwa jicho la tatu kutokana na ubora walionao.

 

Championi Jumamosi limekusogezea orodha ya wachezaji ambao wanatakiwa kuchungwa katika mchezo wa leo kutokana na rekodi ambazo wameziweka mpaka sasa katika Ligi Kuu Bara, ikiwemo katika suala la ufungaji, asisti na uwezo mkubwa wa kufunga kwa faulo.

 

Championi ndio wataalamu wa takwimu za mastaa wa Bongo, hii ni orodha ya wachezaji wachache wa kuchungwa leo;-

 

MEDDIE KAGERE

Huyu ndiye aliyeifunga Yanga kwenye mchezo wa mwisho wa ligi kuu msimu uliopita, ilikuwa Februari 2, mwaka jana katika dakika ya 71 alifunga kwa kichwa bao pekee ambalo Simba waliichapa Yanga pale Uwanja wa Taifa.

 

Tangu msimu huu umeanza, Kagere amecheza mechi 9 na amepachika wavuni mabao tisa pia ametoa asisti mbili. Kagere alifunga dhidi ya JKT Tanzania, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Biashara United, Azam FC, Mbeya City na Lip uli.

 

DAVID MOLINGA- YANGA

Hii itakuwa derby yake ya kwanza tangu ajiunge na Yanga msimu huu. Huyu ni raia wa DR Congo, wakati anatua hakuaminiwa sana na mashabiki wa timu hiyo.

Aliwashtua wengi baada ya kufunga mabao mawili kwenye mechi dhidi ya Polisi Tanzania baada ya hapo ameendelea kuizoea ligi.

 

Mpaka sasa Molinga ‘Falcao’ ameshafunga mabao manne katika Ligi Kuu Bara. Timu alizozifunga ni Polisi Tanzania, JKT Tanzania na Alliance.

Pia ni mpigaji mzuri wa mipira iliyokufa kwani amefunga mabao mawili katika faulo alizopiga ambazo ilikuwa dhidi ya Polisi Tanzania na JKT Tanzania.

 

FRANCIS KAHATA

Kiungo huyo amejiunga na Simba msimu huu akitokea Gor Mahia ya Kenya. Alianza ligi kwa kukaa benchi mara nyingi na leo ni kati ya wachezaji ambao wanatarajiwa kuanza kikosi cha kwanza dhidi ya Yanga.

 

Kahata amehusika katika mabao sita ya Simba, huku yeye akiwa amefunga mawili katika michezo dhidi ya Lipuli na Ndanda FC na ametoa asisti nne katika mechi dhidi ya Azam FC, Ruvu Shooting na KMC.

Kahata ni miongoni mwa wachezaji wazuri wa kupiga mipira iliyokufa, alionyesha uwezo huo dhidi ya Ndanda ambapo alipiga faulo iliyojaa moja kwa moja kambani. Pia ana asisti moja katika mchezo huo.

 

PATRICK SIBOMANA

Mnyarwanda huyu amejiunga na Yanga msimu huu akitokea APR ya Rwanda. Mpaka sasa ameifungia timu hiyo mabao manne katika Ligi Kuu Bara, alitupia dhidi ya Ndanda, JKT Tanzania, Alliance na Tanzania Prisons na ana asisti moja.

 

Pia Sibomana anasifika kwa mipira iliyokufa, anakumbukwa sana kwa bao alilofunga dhidi ya Ndanda FC katika dakika ya 75 baada ya kuupiga mpira uliomshinda Ally Mustapha ‘Barthez’.

 

SHARAF ELDIN SHIBOUB

Kiungo huyo alijiunga na Simba msimu huu akitokea katika timu ya Al-Hilal ya Sudan, anasifika kwa chenga za maudhi pamoja na kuwa na uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira.

 

Tangu Ligi Kuu Bara msimu huu imeanza tayari ameshaingia katika orodha ya wachezaji wa kigeni wa timu hiyo wanaofanya vizuri katika suala la ufungaji na kutoa asisti. Shiboub amehusika katika mabao matatu ya timu hiyo akiwa amefunga bao moja na kutoa pasi mbili za mabao.

 

Shiboub alifunga bao katika mechi dhidi ya Mbeya City katika dakika ya 78 huku akitoa pasi za mabao katika mechi ya Lipuli FC na Mtibwa Sugar.

Abdulghafal Ally, Dar es Salaam

Leave a Comment