×

Mtoto Miaka 11 Adaiwa Kumuua Baba’ake Kisa Kudokoa Mboga

DAR: Ni simanzi Mwaka Mpya 2020! Baba aliyetamani kuuona Mwaka Mpya ambaye ni mkazi wa Goba- Oysterbay jijini Dar, Durban Hassan, anadaiwa kuuawa kwa mpini wa jembe na mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka 11, Gazeti la IJUMAA, lina mkasa mzito.

 

Chanzo cha tukio hilo la kutisha lililojiri maeneo hayo ya Goba, wikiendi iliyopita kinatajwa kuwa ni kitendo cha baba huyo kudokoa mboga ya samaki.

Ilidaiwa kuwa, baba huyo alidokoa kipande cha samaki akala ilihali kilikuwa ni kitoweo cha familia.

 

DADA WA MAREHEMU ASIMULIA

Akilisimulia IJUMAA mkasa huo, dada wa marehemu, Hawa Hassan ambaye ni shangazi wa mtoto huyo alisema kaka yake huyo alikuwa akipokea kipigo mara kwa mara kutoka kwa mkewe ambaye ni mama wa mtoto huyo.

 

Alisema kabla ya tukio hilo baya kwenye familia yao, kaka yake huyo na mkewe walishafikia hatua mbaya kwani kuna siku mkewe huyo alimchoma kisu.

Alisema mara ya kwanza alimchoma tumboni na mara nyingine alimchoma kwenye goti huku akimpiga na mpini wa jembe kichwani mbele ya mtoto wao huyo.

 

“Huyu kaka yangu amekumbana na vipigo vingi sana kutoka kwa mkewe.

“Alishafikia hatua ya kumpa talaka, lakini kwa vile alikuwa akitaka nyumba ya mdogo wangu, alikuwa mara kwa mara anarudi nyumbani kinyemela.

“Lakini ilikuwa akikosana tu na mdogo wangu, basi anampiga sana kwa sababu alishamuona dhaifu kutokana na kumwaga damu mara kwa mara,” alisema dada huyo wa marehemu.

 

SIKU YA TUKIO

Dada huyo aliendelea kusimulia kuwa, siku ya tukio, kaka yake huyo alikuwa ametoka kwenye mizunguko yake na kurudi nyumbani ambapo alimkuta mtoto wake huyo akiwa ameandaa samaki vipande vitatu.

Alisema, kaka yake huyo alichukua kipande kimoja akala na hapo ndipo ugomvi ulipoanzia ambapo mtoto huyo alichukua mpini na kumpiga kichwani.

 

Alisema kufuatia tukio hilo, kaka yake alitokwa na damu nyingi zilizokuwa zinaruka kama maji kutoka kwenye jeraha la kichwani.

“Kwa mujibu wa majirani walio karibu, mtoto huyo wa kaka yangu ndiye aliyempiga baba yake na wakati akihojiwa alikiri hivyo.

 

“Basi, baada ya kuona hali ile, majirani walimchukua kaka yangu na kumpa huduma ya kwanza.

“Kaka yangu aliendelea kuuguza jeraha mwenyewe nyumbani kwani mkewe alipopigiwa simu kuelezwa tukio hilo, alichojibu ni kwamba mtoto huyo angemuua kabisa baba yake,” alisema dada huyo.

 

JUMAPILI ILIYOPITA

Aliendelea kusema kuwa, baada ya kupata jeraha hilo, kaka yake aliendelea kuugulia maumivu tangu Ijumaa iliyopita hadi Jumapili ambapo alitoka kupiga stori na wenzake, aliporudi nyumbani kulala, muda mfupi baadaye alifika mkewe huyo akimtafuta.

Alisema mwanamke huyo alipoingia ndani alitoka haraka na kuanza kuomba msaada kwani alisema haielewielewi hali ya mumewe huyo.

 

“Hadi sasa tupo kwenye sintofahamu kwa sababu muda mfupi tu baada ya mkewe kuonana naye, ndipo akawapa taarifa za kuwa amezidiwa na hata majirani walipokwenda kumuangalia waliingiwa na wasiwasi.

Alisema baada ya hapo alichukuliwa na kukimbizwa kwenye Hospitali ya Goba ambapo waliambiwa wampeleke Hospitali ya Massana iliyopo njia panda ya Goba.

 

Alisema kuwa, alipofikishwa hospitalini hapo na kupimwa, aligundulika ameshafariki dunia.

“Kilichofuata baada ya hapo ni kuchukua mwili na kwenda kuuhifadhi Hospitali ya Lugalo ili kufanya taratibu za mazishi,” alisema dada huyo kwa uchungu.

 

KAMANDA KINONDONI

Akizungumza na Gazeti la IJUMAA juu ya tukio hilo, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Musa Taibu alisema kuwa, mwanzo wa tukio hilo liliripotiwa kama shambulio la kudhuru mwili, lakini kwa sababu baba huyo alifariki dunia, basi litakuwa ni tukio la mauaji.

“Nitazidi kulifuatilia tukio hilo kwa undani, halafu nitawajulisha zaidi nini kinaendelea,” alisema Kamanda Taibu.

Stori: IMELDA MTEMA NA KHADIJA BAKARI, Ijumaa

Leave a Comment