
Dar es Salaam, Tanzania – Jumatano, 4Septemba 2025: Stanbic Bank Tanzania imeahidi jumla ya TZS 100 milioni kwenye kampeni ya Afya Check, hatua inayotarajiwa kupanua huduma za kiafya zitolewazo bure kwa maelfu ya wananchi nchini ambao wanakabiliwa na changamoto za kupata matibabu kwa wakati.
Mchango huo utawezesha kambi za afya na shughuli za uhamasishaji katika mikoa minne, na kupanua programu ambayo tayari imewafikia zaidi ya wakazi 48,000 katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mwanza, Arusha, Pwani, Tanga, Zanzibar na Mbeya tangu mwaka 2022.

Mpango wa Afya Check Community Outreach unalenga kugundua magonjwa mapema, kutoa elimu ya afya na tiba bure kama vile uchunguzi wa saratani, huduma za meno na macho, ushauri nasaha wa VVU, chanjo na kutoa rufaa kwenda hospitali kubwa.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009, mpango huu umehudumia zaidi ya nusu milioni ya Watanzania.
Annette Nkini, Meneja Uendelevu wa Benki ya Stanbic Bank, alisema mchango huu unaonesha dhamira ya Benki ya kuhakikisha ustawi wa jamii kwa muda mrefu.

“Kwa kuunga mkono Afya Check kwa TZS 100 milioni mwaka huu, tunasaidia kuendesha kambi nne za afya katika mikoa minne.
Hatua hii inaonesha kujitolea kwetu kujenga jamii zenye afya bora, ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu ya Taifa. Tunajivunia kushirikiana na taasisi ambayo tayari imewafikia zaidi ya nusu milioni ya watu kwa huduma bure za kiafya, na tunaamini kwapamoja tutawafikia watu wengi zaidi,”alisema.

Afya Check imejikita kama daraja kwa watu wasioweza kumudu huduma za matibabu kwa wakati, hasa ikijibu ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, changamoto za afya ya akili na ulemavu.
Kambi zake za afya hukusanya madaktari, wataalam, wauguzi na wafamasia, kwa kushirikiana na hospitali za serikali na binafsi.
Ushirikiano huu na Stanbic Bank pia utahusisha programu za uhamasishaji mashuleni na kuendeleza mifumo ya kidigitali ya kuhamasisha tabia za kujikinga kiafya. Waandaaji wanaamini hatua hizi zitasaidia kuunda mienendo bora ya kiafya na kuongeza usimamizi mzuri wa kiafya katika jamii mbalimbali nchini.
Kwa Afya Check, uwezeshaji huu unamaanisha upanuzi wa huduma za kiafya zitakazoleta athari chanya kwenye jamii. “Ushirikiano huu na Stanbic Bank ni hatua kubwa ya kuhakikisha watu wengi zaidi wananufaika na huduma bure za kiafya.
Kwa pamoja tunajenga utamaduni mzuri wa watu kufanya uchunguzi wa afya zao mapema nchini Tanzania,”alisema Dkt. Isaac Maro Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Afya Check.
Mchango huu mpya unaendeleza rekodi ya uwekezaji mpana wa kijamii wa Stanbic Bank. Tokea Januari 2025, benki ilitoa viti 50 vya Bengal kwa Shule ya St Jude, ilioyoko Arusha kusaidia zaidi ya wanafunzi 1,800 wanaotoka kwenye familia zenye kipato cha chini kupata elimu bora.
Mbeya, benki ilitoa madawati 100 kwa shule za sekondari na kupanda miche 200 ya matunda na kivuli kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira.
Zaidi ya elimu na mazingira, programu za kijamii za Stanbic Bank ziliwafikia zaidi ya watu 100,000 mwaka 2024 pekee, zikihusisha afya, ujasiriamali wa vijana, uwezeshaji wa wanawake na elimu ya kidigitali.
Benki imedhamini kliniki za afya za simu kwa jamii zenye uhitaji mkubwa, kusaidia wanawake wajasiriamali kwa mikopo midogo na ushauri wa kibiashara, na kupanda zaidi ya miti 50,000 nchini kote kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuhamasisha maisha endelevu.
Mwaka huu benki ya Stanbic inaadhimisha miaka 30 tangu ianze shughuli zake nchini Tanzania. Maadhimisho haya yanaonesha urathi wa benki kwenye usimamizi wa rasilimali fedha, ubunifu, na kujitolea kwa maendeleo ya Taifa.
Benki ya Stanbic huko mbeleni, inaendelea kuchangia ukuaji wa kifedha, uwekezaji kwenye jamii. Hii inathibitisha kuwa ushirikiano thabiti na jamii ndio msingi wa kujenga na Tanzania yenye afya bora, jumuishi na endelevu.