
MANCHESTER United juzi walimpoteza beki wao mahiri Harry Maguire ambaye alikumbana na majeraha wakati ambapo timu hiyo inatakiwa kujidhatiti vizuri sana.
Huu siyo mwezi mzuri kwa United kutokana na ratiba yao kuwa na michezo mingi sana mikubwa.
United watakuwa na ratiba ngumu sana kwa kipindi hiki cha Januari na kuna mambo mawili yanaweza kutokea.
Moja inaweza kuwa kipindi ambacho United wataamka na kuwa timu imara zaidi England, au kinaweza kuwa kipindi cha mwisho kabisa cha umaarufu wa timu hiyo msimu huu.
Mwezi huu United wanaweza kuendelea kwenda Kombe la FA au kuondolewa, wanaweza kuendelea kwenye Kombe la Carabao Cup au kuondolewa na wanaweza kujiweka sawa kwenye ligi au kupoteza matumaini kabisa.
Kitendo cha beki huyo mahiri ambaye amecheza kwenye michezo karibia yote ya timu hiyo msimu huu kuumia kinaonyesha kuwa kunaweza kuwa ni pigo kubwa zaidi kwa vijana hao wa jiji la Manchester.
Pia timu hiyo inakuwa na pigo kwa kuwa tena haina mabeki wake watano ambao wanasumbuliwa na majeraha na labda iwe bahati kwa timu hiyo kama watarejea wachache.
Lakini pia wachezaji wake wawili mahiri, Anthony Martial na Jesse Lingard nao wana majeraha madogomadogo na hivyo wanaweza wasicheze michezo yote.
Timu hiyo itakuwa na michezo sita mikubwa na hiyo miwili itakuwa dhidi ya wapinzani wao wakubwa Manchester City kwenye hatua ya nusu fainali ya Carabao Cup.
Mchezo wa kwanza wa timu hiyo ulikuwa jana dhidi ya City ambapo Man U walifungwa bao 3-1 tena wakiwa nyumbani, katika Dimba la Old Traford.
Kabla ya mchezo dhidi ya Wolves, United ilisema kuwa wachezaji wa timu hiyo Axel Tuanzebe, Marcos Rojo, Eric Bailly na Timothy Fosu-Mensah walikuwa wanasumbuliwa na majeraha.
Hii inaonyesha kuwa kama wachezaji hao watakosekana kwenye michezo mingine ijayo utakuwa mzigo mkubwa kwa timu hiyo inayowania angalau kombe moja msimu huu.
Mbali na mechi kali dhidi ya Manchester City, Manchester United ratiba yao inaonyesha kuwa watakuwa na mechi kali dhidi ya Liverpool, Jumapili ya Januari 19 mwaka huu.
Huu ni mchezo wa Ligi Kuu England ambao unaweza kuwa daraja la Liverpool kutwaa ubingwa wa ligi hiyo au unaweza kuwa sababu ya timu hiyo kupunguzwa kasi ya kuwania ubingwa huo.
Mchezo wa marudio dhidi ya City ndiyo utakuwa wa mwisho kwa timu hiyo mwezi huu ambapo utapigwa Januari 29.
“Tupo kwenye kipindi cha Januari, mara nyingi ni kipindi ambacho kila timu huwa na ratiba ngumu.
“Tunakwenda kwenye michezo kadhaa migumu, tutakutana na Manchester City, Liverpool na hata Wolves, nafikiri ni kipindi ambacho lazima tukubali kuongeza juhudi ili kuona ni jambo gani tunaweza kuvuna mwishoni mwa msimu huu.
“Pamoja na mambo mengine, lakini tumejiandaa kupambana kuhakikisha kuwa tunaweza kufanya jambo kwa kipindi hiki,” alisema kocha wa United, Ole Gunnar Solskjaer.
Mbali na mechi hizo kubwa, pia United watavaana na Burnley kwenye Ligi Kuu England pamoja na Norwich City.
Kwenye Kombe la FA, timu hiyo itakutana na Wolves, Januari 14.
Bado United hawapo vizuri sana kwenye Ligi Kuu England wakiwa wanashika nafasi ya tano baada ya kucheza michezo 21, wakiwa wameshinda michezo nane wametoka sare saba na kupoteza michezo sita.
Timu hiyo imefanikiwa kukusanya pointi 31 ikiwa imefunga mabao 32 na kufungwa 25.
MANCHESTER, England